Maafisa wa Usalama wa Ndani wa Marekani wamefanya msako katika nyumba ya mbunge wa chama cha Democratic, Ilhan Omar, jijini Washington, kabla ya mapambazuko.

Taarifa zinasema kuwa hati ya upekuzi inahusiana na uchunguzi kuhusu nyaraka za uhamiaji ambazo baba yake aliwasilisha kwa niaba yake alipokuwa mtoto.

Mwezi uliopita, Tom Homan, afisa wa Ikulu ya Marekani anayesimamia masuala ya mpaka, alithibitisha kuwa Omar alikuwa akichunguzwa katika makosa ya jinai. Omar amewahi kukanusha madai ya Rais Donald Trump kwamba uraia wake ulipatikana kwa njia ya udanganyifu, akisema mashambulizi yake ya mara kwa mara dhidi yake yana nia za kisiasa.

Omar alizaliwa nchini Somalia na alifika Marekani akiwa na umri wa miaka nane, akikimbia vita. Alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa mbunge wa Congress mwaka 2018, na amekuwa mkosoaji mkubwa wa Rais Donald Trump.

Kwa sasa, Bunge la Marekani halifanyi vikao, na haijulikani iwapo Omar alikuwa nyumbani wakati wa msako huo.

BBC imewasiliana na Omar ili kupata maoni yake kuhusu tukio hilo.