LAGOS: Rais wa Nigeria, Bola Tinubu, ametangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa baada ya ndege ya kijeshi kuanguka katika Jimbo la Ondo, kusini mwa nchi hiyo na kusababisha vifo vya watu 32 Oktoba 9, 2026.

Ndege hiyo ilikuwa na abiria 25 na wahudumu saba ikiwa katika safari ya kawaida kutoka Benin City kuelekea Lagos Jumatatu asubuhi, kabla ya kuanguka karibu na kituo cha jeshi la majini katika eneo la Igbokoda, Ondo.

Mkazi mmoja akizungumza na chombocha habari amesema ndege hiyo ilianguka katika eneo lenye kinamasi, huku nguo na viatu vikionekana katika eneo la ajali na moshi ukiendelea kuonekana ukipanda kutoka eneo hilo.

Rais Tinubu ametoa pole kwa familia za waliofariki na kuamuru uchunguzi wa kina ufanyike ili kubaini chanzo cha ajali hiyo na kuzuia matukio kama hayo kutokea tena.

Aidha, ameagiza bendera za taifa kushushwa hadi nusu mlingoti kote nchini kama ishara ya heshima kwa waliopoteza maisha.

“Huu ni wakati wa maumivu kwa Majeshi yetu na taifa zima,” amesema Tinubu, akiongeza kuwa wanajeshi wa Jeshi la Anga la Nigeria huweka maisha yao hatarini kila siku katika kulinda usalama wa nchi.

Waziri wa Usafiri wa Anga wa Nigeria, Festus Keyamo, amesema awali alipokea taarifa kuhusu kupotea kwa mawasiliano na ndege hiyo yenye namba ya mkia NGR 931, iliyokuwa ikielekea Lagos kutoka Benin City.

Keyamo amesema juhudi za kuwasiliana na ndege hiyo kupitia redio hazikufanikiwa, kabla ya kuthibitishwa baadaye kuwa ilikuwa imeanguka karibu na kituo cha jeshi la majini huko Igbokoda.

Ndege hiyo imetajwa kuwa aina ya ATR-42, ambayo kwa mujibu wa watengenezaji wake inaweza kubeba kati ya abiria 30 na 50.

Majina ya waliofariki bado hayajatangazwa rasmi, huku mamlaka zikisema utambulisho wa maafisa waliokuwamo kwenye ndege hiyo utatolewa baada ya familia zao kupewa taarifa.

Ajali hiyo ni miongoni mwa ajali mbaya zaidi za ndege nchini Nigeria katika miaka ya hivi karibuni.

Mwaka 2021, Mkuu wa Jeshi la Nigeria wakati huo, Luteni Jenerali Ibrahim Attahiru, alifariki pamoja na maafisa wengine 10 baada ya ndege yao kuanguka katika Jimbo la Kaduna.

Mwaka huo huo, watu saba walifariki baada ya ndege ya kijeshi kuanguka karibu na njia ya kutua katika mji mkuu Abuja.