Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ametangaza mabadiliko katika Baraza la Mawaziri, hatua inayokamilisha uundwaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa kuwajumuisha viongozi kutoka Chama cha ACT-Wazalendo.

Mabadiliko hayo yametangazwa leo, Oktoba 3, 2026, katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Ikulu Zanzibar.

Katika mabadiliko hayo, ACT-Wazalendo imepata nafasi nne za uwaziri.

Mawaziri hao ni Nassor Ahmed Mazrui, aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Afya; Omar Said Shaaban, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda; Dkt. Nasra Nassor Omar, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale; pamoja na Dkt. Mohamed Ali Suleiman, Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu.

Aidha, Rais Mwinyi ametangaza mabadiliko ya muundo wa baadhi ya Wizara, ikiwa ni pamoja na kuhamishia masuala ya Mipango katika Ofisi ya Rais, Ikulu, pamoja na kuanzishwa kwa Wizara ya Kazi, Ajira, Vijana na Uwezeshaji.

Katika mabadiliko hayo, Shaaban Ali Othman ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu, anayeshughulikia Mipango na Usimamizi wa Utendaji Serikalini.

Masoud Ali Mohamed ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu, anayeshughulikia Uhusiano wa Jamii.

Mudrik Ramadhan Soraga amepewa nafasi ya Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, huku Ali Suleiman Ameir Mrembo akiteuliwa kuwa Waziri wa Kazi, Ajira, Vijana na Uwezeshaji.

Mabadiliko hayo pia yamewagusa Naibu Mawaziri katika Wizara mbalimbali, zikiwemo Afya, Kilimo, Elimu, Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Fedha, Utalii na Mambo ya Kale, pamoja na Kazi, Ajira, Vijana na Uwezeshaji.

Akizungumza wakati akitangaza mabadiliko hayo, Rais Mwinyi amesema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano ya maridhiano kati ya CCM na ACT-Wazalendo kuhusu uundwaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Mawaziri na Naibu Mawaziri wote walioteuliwa na waliohamishwa wanatarajiwa kuapishwa Jumatatu, Oktoba 5, 2026, saa 8:00 mchana.