Rais wa Kenya William Ruto ameagiza Kamati ya Baraza la Kitaifa la Usalama kufanya tathmini ya hali ya Ebola nchini humo na kupendekeza hatua zaidi za kukabiliana na ugonjwa huo, baada ya kifo cha mgonjwa wa kwanza aliyethibitishwa kuwa na virusi hivyo.

Mgonjwa huyo, raia wa Kenya aliyewasili kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kupitia Uganda, alipatikana na virusi vya Ebola aina ya Bundibugyo.

Hadi sasa, mamlaka zinasema hakuna visa vingine vilivyothibitishwa. Maafisa wa afya wamesema abiria 27 waliokuwa kwenye ndege iliyosafiri kutoka Kampala hadi Nairobi wametambuliwa au wamewasiliana na mamlaka kwa ajili ya ufuatiliaji.

Wakati huo huo, wanafamilia wanane wa marehemu pamoja na wahudumu 21 wa afya waliokuwa wamehudhuria matibabu yake wamewekwa karantini na wanafuatiliwa kwa siku 21 ili kubaini iwapo watapata dalili zozote za ugonjwa huo.

Mamlaka zinasema hatua za ufuatiliaji na kudhibiti maambukizi zinaendelea huku zikiwataka wananchi kuendelea kuwa watulivu na kufuata ushauri wa wataalamu wa afya.