Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limepokea silaha aina ya gobore 68 kutoka kwa wananchi walioitikia wito wa kusalimisha silaha hizo katika kipindi cha msamaha kinachoendelea hadi Oktoba 31, 2026.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Almachius Mchunguzi, amesema mwitikio wa wananchi umekuwa mkubwa kutokana na elimu inayotolewa na Jeshi hilo kuhusu umuhimu wa kusalimisha silaha hizo.
Amesema baadhi ya wananchi wamekuwa wakizifikisha wenyewe katika vituo vya Polisi kwa ajili ya kuzisalimisha, hatua inayowapa fursa ya kutekeleza wito huo ndani ya kipindi cha msamaha na kuepuka kuchukuliwa hatua za kisheria baada ya muda huo kumalizika.
Aidha, Kamanda Mchunguzi amewataka wananchi wa Mkoa wa Tanga kuacha kujihusisha na utengenezaji wa silaha aina ya gobore, akisisitiza kuwa utengenezaji na umiliki wa silaha hizo ni kinyume cha sheria.
Amewataka pia wananchi wenye taarifa kuhusu watu wanaojihusisha na utengenezaji wa silaha hizo kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa.
.jpeg)
.jpeg)

0 Comments