Cristiano Ronaldo amerejea kwa kishindo katika kikosi cha Al-Nassr kwa kufunga bao na kuiongoza timu yake kupata ushindi, siku chache baada ya kuzua mjadala kufuatia kuondoka kambini mwa timu ya taifa ya Ureno.
Nahodha huyo wa Ureno mwenye umri wa miaka 41 aliondoka kambini wakati wa mapumziko ya mechi za Ligi ya Mataifa baada ya kubaki benchi katika mchezo dhidi ya Norway. Hata hivyo, amesisitiza kuwa hajaaga soka la kimataifa, licha ya kumkosoa kocha Jorge Jesus kwa kile alichokiita "uvunjifu mkubwa wa imani".
Kabla ya mchezo wa Ligi Kuu ya Saudi Arabia dhidi ya Diriyah, mashabiki wa Al-Nassr walimkaribisha Ronaldo kwa kuonyesha bango kubwa lililosomeka: "Ukuu hupatikana kwa juhudi, CR7, mfungaji bora wa muda wote katika historia ya soka."
Ronaldo aliwathibitishia imani hiyo mashabiki wake kwa kuifungia Al-Nassr bao la kwanza katika dakika ya 23, akimalizia mpira uliotemwa na kipa baada ya kuokoa shuti la Kingsley Coman.
Bao hilo lilikuwa la 980 katika maisha yake ya soka akiwa amezichezea Sporting CP, Manchester United, Real Madrid, Juventus, Al-Nassr na timu ya taifa ya Ureno.
Nyota huyo sasa anasalia mabao 20 pekee kufikia rekodi ya mabao 1,000 katika mechi rasmi, mafanikio ambayo hayajawahi kufikiwa na mchezaji yeyote katika historia ya mchezo huo.
Kati ya mabao hayo, 146 ameyafunga akiwa na timu ya taifa ya Ureno katika mechi 234, rekodi zinazomfanya kuwa mfungaji bora na mchezaji aliyeichezea zaidi timu ya taifa katika soka la kimataifa la wanaume.
Al-Nassr iliendelea kutawala mchezo huo baada ya Samu Costa kufunga bao la pili kwa kichwa akimalizia kona ya João Félix, kabla ya Kingsley Coman kuhitimisha ushindi huo kwa bao la tatu katika dakika ya 77.

0 Comments