Rais wa Kenya, William Ruto, anaongoza maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Mazingira ya mwaka huu katika Elgon Downs, Endebess, Kaunti ya Trans Nzoia, huku serikali ikiongeza kasi ya utekelezaji wa mpango wa kupanda miti bilioni 15 kufikia mwaka 2032.

Maadhimisho hayo yanafanyika wakati mjadala kuhusu uhifadhi wa misitu ukiendelea kushika kasi, kufuatia wasiwasi ulioibuliwa na wadau wa mazingira kuhusu ukataji wa miti mikubwa katika baadhi ya misitu nchini.

Wiki ya Mazingira ya mwaka huu, iliyoanza Oktoba 5, inalenga kupandwa kwa miti milioni 17.24 kupitia ushiriki wa jamii, shule, taasisi za umma na wadau wengine wa uhifadhi wa mazingira.

Katika juhudi za kuhamasisha wananchi kushiriki zaidi katika urejeshwaji wa uoto wa asili, serikali pia imeandaa kampeni ya Green Challenge, inayolenga kuwahamasisha Wakenya 200,000 kupanda miti milioni sita ndani ya saa moja siku ya Jumamosi.

Serikali inaeleza kuwa kampeni hiyo ni sehemu ya mkakati mpana wa kuongeza eneo la misitu, kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha uhifadhi wa mazingira nchini.