Mahakama Kuu ya Saudi Arabia imebatilisha hukumu ya kifo iliyokuwa imetolewa dhidi ya mfanyakazi mhamiaji kutoka Sri Lanka, Anojan Sivarasa, baada ya kupatikana na hatia ya kukufuru kwa kumtusi Mtume Muhammad kupitia maoni aliyochapisha kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Sri Lanka, Arun Hemachandra, alitangaza uamuzi huo akisema mahakama hiyo ilifuta hukumu hiyo siku ya Jumatano. Aliishuku mamlaka na timu za kisheria za mataifa yote mawili kwa juhudi zao katika kushughulikia kesi hiyo.
Sivarasa, mwenye umri wa miaka 27, alihukumiwa kifo mwezi Septemba baada ya mahakama ya rufaa nchini Saudi Arabia kumtia hatiani kwa kosa hilo. Kesi hiyo ilizua mshtuko mkubwa nchini Sri Lanka na kusababisha juhudi za kidiplomasia za kuomba msamaha.
Chanzo cha tukio hilo kinahusishwa na mjadala mkali uliozuka kwenye mitandao ya kijamii mwishoni mwa Juni, baada ya kusambaa kwa video ikimuonyesha kijana mmoja Muislamu akimpiga teke mbwa aliyekuwa akiwafuata mahujaji wa Kihindu. Mjadala huo ulisababisha mabishano ya kidini mtandaoni.
Katika mabadilishano hayo ya ujumbe, mtumiaji mmoja alitoa kauli za kumdhalilisha mungu wa Kihindu, jambo lililomfanya Sivarasa kujibu kwa lugha ya Kitamil kwa maneno yaliyomkashifu Mtume Muhammad.
Ingawa baadaye alifuta maoni hayo na kuchapisha video ya kuomba radhi, picha ya skrini ya ujumbe huo ilifikishwa kwa mwajiri wake na maafisa wa Saudi Arabia, hatua iliyosababisha kukamatwa kwake mwezi Julai.
Haijabainika ikiwa atachukuliwa hatua nyingine za kisheria au kama Sivarasa ataendelea kuzuiliwa, na kwa muda gani. Awali, Mahakama ya Jinai ya Al-Ahsa ilikuwa imemhukumu kifungo cha miaka mitano gerezani pamoja na faini ya riyal milioni tatu za Saudi Arabia.

0 Comments