.jpeg)

Tanzania yang'ara nchini Algeria kufuatia kupewa hadhi ya kuwa mgeni wa heshima katika maonesho ya kimataifa ya ujenzi, makaazi na miradi ya miundombinu yalijulikanayo kama Bati-Est Expo 2026, jijini Constantine, Algeria.
Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Mobhare Matinyi ndiye aliyeiwakilisha Tanzania katika maonesho hayo ya tisa yanayofanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 14 Oktoba, 2026, akiambatana na Gavana wa Constantine, Kerbouch Kamel, katika sherehe rasmi za ufunguzi.
Akizungumza na Shirika la Habari la Algeria (APS), Balozi Matinyi amewaomba wawekezaji na wafanyabiashara wa sekta ya ujenzi nchini Algeria kuja Tanzania kwa kuzingatia ushirikiano mzuri uliopo baina ya nchi hizi mbili na fursa nyingi zilizopo nchini.
Sekta ya ujenzi nchini Tanzania inachangia takriban asilimia 13 ya pato la taifa na inakua kwa wastani wa asilimia 10 kwa mwaka, alidokeza Balozi Matinyi huku akisisitiza kwamba Tanzania ni nchi rafiki kwa wawekezaji na wafanyabiashara.
Akielezea zaidi, Balozi Matinyi alisema, Tanzania ina miradi mingi ya ujenzi na ipo kwenye eneo linalounganisha kanda za mashariki, kati na kusini mwa Afrika, huku ikiwa ni nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), hivyo kuwa kitovu cha biashara kikanda.”
Katika eneo hili, kama ilivyo kwenye sekta zingine muhimu, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka mkazo maalum kwenye kutanua fursa za uwekezaji katika tasnia ya ujenzi, ambayo kwa sasa inashuhudia ukuaji mkubwa, na hivyo kuongeza mitaji kutoka nje, alidokeza balozi.
Aliongeza zaidi kuwa, kwa kutambua uzito wa sekta hii katika kukuza uchumi, Rais Samia ameongeza fursa za uwekezaji nchini Tanzania kutoka Afrika na duniani, hivyo, kufungua milango zaidi katika sekta hii.
Miradi ya kimkakati inayoendelea nchini hivi sasa kiujumla iliyotajwa na balozi ni ujenzi na upanuzi wa bandari na viwanja vya ndege, reli ya kisasa (SGR) inayokwenda nchi jirani, mtandao wa barabara nchini, majengo ya makaazi na huduma za jamii kama hospitali na shule, hoteli za kitalii, viwanja vya michezo na miradi ya maji na umeme.
Balozi Matinyi aliongeza kuwa mbali ya miradi hii mikubwa ya kimkakati lakini bado pia serikali inaendelea kuujenga mji mkuu mpya wa Dodoma ambao utakuwa na uwanja wa ndege wa kimataifa wa nne nchini Tanzania baada ya vile vya Dar es Salaam, Kilimanjaro na Zanzibar.
Vilevile, Ubalozi wa Tanzania nchini Algeria ulipata fursa ya kuzungumza na kampuni kadhaa zilizoonesha nia ya kuja Tanzania kutafuta fursa za uwekezaji na ubia na wenzao katika kuzalisha na kuuza vifaa vya ujenzi, kushiriki kwenye miradi ya ujenzi na kununua malighafi kutoka Tanzania.
Baadhi ya kampuni hizo ni ERCM Salhi ya ujenzi wa kisasa wa kutumia vyuma, Mirage Landmark ya ujenzi wa makaazi ya maghorofa, kampuni za milango ya kisasa za DEI na Fhaima, kampuni za rangi za ENAP, Julex Color na Semin Algerie, kampuni ya uzio wa chuma ya Atom Metal na kampuni ya nyasi bandia ya Golden Grass.
Maonesho hayo yaliyosimamiwa na kampuni ya Sunflower yalijumuisha washiriki 167 wengi wakitokea Algeria pamoja na washiriki wengine kutoka Uturuki, Ujerumani, Uingereza, Tunisia na Misri.
Mapema kabla ya maonesho ya Constantine, mnamo tarehe 13 Oktoba, 2026, Balozi Matinyi alitembelea Maonesho ya Nne ya Kimataifa ya Uwekezaji na Teknolojia ya Kilimo jijini Annaba (Agritech Expo Annaba 2026), ambapo pia alipata fursa ya kufanya vikao na kampuni za Algeria zenye nia ya kuwekeza na kufanya biashara nchini Tanzania.
Kampuni hizo zinajumuisha New Fertilizers na Agrosafia za mbolea; Biotec-in ya lishe, afya na uzalishaji wa mifugo; Alviar inayotaka ngombe kutoka Tanzania; na Giplait ya bidhaa za maziwa. Zingine ni Weetel Water ya kugeuza unyevu wa angani kuwa maji; Treox na Aquaox za kusafisha maji kwa kutumia teknolojia ya chumvi na umeme; na Sofood Sogood ya Chad ya kubangua korosho.
Maonesho hayo ya nne yaliyofanyika kuanzia tarehe 13-15 Oktoba, 2026, na yalisimamiwa na kampuni ya Incop yakijumuisha washiriki 117 kutoka kampuni za ndani na nje ya Algeria.
0 Comments