Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza, Shabana Mahmood, ametishia kuwapiga marufuku Waeritrea wote kuingia nchini humo iwapo serikali ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki haitakubali kurejeshwa kwa wahamiaji wengi zaidi walioingia Uingereza kwa boti ndogo na wahalifu ambao ni raia wa kigeni.

Kuanzia Alhamisi, wanadiplomasia wa Eritrea watakabiliwa na vikwazo vya kutembea nje ya London. Pia, huduma ya kutoa visa za haraka kwa watu mashuhuri na viongozi itasitishwa.

Hapo awali, mawaziri wa Uingereza wameishinikiza nchi nyingine kukubali kuwapokea raia wao wanaorejeshwa kwa kutishia kuzipiga marufuku visa zao.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka Maktaba ya Bunge la Uingereza, Waeritrea walikuwa kundi kubwa zaidi la wahamiaji walioingia nchini humo kwa boti ndogo katika kipindi cha miezi 12 hadi Juni, wakichangia asilimia 18 ya waliowasili.

“Eritrea imepewa kila fursa ya kukubali kuwarejesha wahalifu na watu wasio na haki ya kuendelea kuwa nchini Uingereza. Tofauti na nchi nyingine, imekataa,” alisema Mahmood.

Alisema hatasita “kuchukua hatua zaidi dhidi ya nchi nyingine zinazokataa kushirikiana”.

Serikali ya Uingereza imeituhumu serikali ya Eritrea kwa kusitisha ghafla ushirikiano mapema mwaka huu.

Chini ya vikwazo hivyo, wanadiplomasia wa Eritrea hawataruhusiwa kusafiri umbali wa kilomita 60 nje ya London bila kupata kibali.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uingereza imesema hatua hiyo inafanana na vikwazo vinavyowekwa kwa maafisa wa Uingereza katika mji mkuu wa Eritrea, Asmara.

Dkt Madeleine Sumption, mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Uhamiaji katika Chuo Kikuu cha Oxford, amesema kuilenga Eritrea hakutakuwa na athari kubwa.

Ubalozi wa Eritrea mjini London umeombwa kutoa maoni kuhusu suala hilo.