Rais wa Marekani Donald Trump amefuta mpango wa kurusha mubashara kwenye mtandao utekelezaji wa hukumu ya kifo kwa Nidal Hasan, aliyekuwa daktari wa magonjwa ya akili katika jeshi la Marekani, kwa kupigwa risasi na kikosi cha kufyatua risasi.
Trump awali alisema aliunga mkono kurushwa kwa video ya kuuawa kwake kupitia mtandao, huku Makamu wa Rais JD Vance akitilia shaka iwapo hatua hiyo ingetekelezwa na kusema kwamba yeye hataitazama.
Huku ukosoaji kuhusu kuoneshwa hadharani kwa tukio hilo ukiongezeka, Trump alisema Alhamisi kwamba “watu wengi wazuri wenye nia njema wangependelea kutomtazama akifa”.
“Nadhani kurusha mubashara utekelezaji wa hukumu hiyo ili kila mtu aone kungeweza kuwa kizuizi kikubwa, huku dunia ikishuhudia jinsi Marekani inavyowashughulikia magaidi na watu wachafu kama Hasan,” Trump alisema.
“Anapaswa kufa kama ilivyopangwa, kwa kupigwa risasi na kikosi cha kufyatua risasi, lakini tukio hili halitarushwa mubashara,” rais huyo aliongeza.
Hasan aliwaua kwa kuwapiga risasi wanajeshi 13 wa Marekani ambao hawakuwa na silaha katika kambi ya kijeshi huko Texas mwaka 2009, na kuwajeruhi wengine 32. Utekelezaji wa hukumu yake ya kifo kwa kikosi cha kufyatua risasi utakuwa wa kwanza kwa jeshi la Marekani katika kipindi cha zaidi ya miaka 60.
Trump alisema familia za wahanga zitaruhusiwa kushuhudia utekelezaji huo wa hukumu ya kifo ana kwa ana.
“Wanastahili kushuhudia HAKI IKITENDEKA!” Trump alisema.
Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) ilitangaza wiki iliyopita kuwa Hasan atauawa kwa kupigwa risasi na kikosi cha kufyatua risasi tarehe 3 Desemba 2026.
Baadaye, Waziri wa Ulinzi Pete Hegseth alisema tukio hilo lingerushwa mubashara ili umma uweze kulitazama, akiongeza kuwa “watu wanahitaji kuelewa kwamba vitendo vya aina hii vina matokeo makubwa”.
Hasan alifyatua risasi katika jengo la matibabu lililokuwa na watu wengi, ambako wanajeshi waliokuwa wakijiandaa kwenda kwenye operesheni za kijeshi walikuwa wakingojea kufanyiwa uchunguzi wa afya na kupatiwa chanjo.
Baadaye, alikiri mahakamani kuwa ndiye aliyefyatua risasi na akaomba radhi kwa “makosa yoyote” aliyoyafanya.
Wakati wa kesi yake ya kijeshi mwaka 2013, alisema aliamini kwamba alikuwa akiwalinda Waislamu na kundi la Taliban nchini Afghanistan dhidi ya jeshi la Marekani.
Mauaji hayo, yaliyotokea tarehe 5 Novemba 2009, yalikuwa shambulio baya zaidi kuwahi kutokea katika kambi ya kijeshi ya Marekani wakati ambapo hakukuwa na mapigano.

0 Comments