MWANZA; Serikali imesisitiza umuhimu wa kukamilisha kwa wakati ujenzi wa hospitali yenye hadhi ya rufaa katika Wilaya ya Ukerewe, Mkoa wa Mwanza, ili kuwawezesha wananchi kupata huduma za kibingwa na kibingwa bobezi bila kulazimika kusafiri umbali mrefu kutafuta matibabu.

Akizungumza leo wakati wa kukagua maendeleo ya ujenzi wa hospitali hiyo wilayani Ukerewe, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Paul Makonda amesema utekelezaji wa mradi huo umefikia zaidi ya asilimia 50 na unatarajiwa kukamilika Februari 2027, ambapo wananchi wataanza kupata huduma za matibabu.

Makonda amesema ujenzi wa hospitali hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kusogeza huduma bora za afya karibu na wananchi, hususan wakazi wa Ukerewe ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma za kibingwa.

“Hospitali hii itakuwa na hadhi ya kutoa huduma za kibingwa na kibingwa bobezi, pamoja na vifaa tiba vinavyohitajika ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya,” amesema.

Amesema uamuzi wa kujenga hospitali hiyo unatokana na dhamira ya kutimiza ahadi iliyotolewa kwa wananchi wa Ukerewe, ambao wanahitaji huduma bora za afya zinazopatikana kwa urahisi.

Aidha, amesema utekelezaji wa mradi huo unaonesha umuhimu wa viongozi kusimamia ahadi wanazozitoa kwa wananchi na kuhakikisha zinageuzwa kuwa matokeo yanayoonekana.

Makonda amesema hospitali hiyo ina uwezo wa kuvutia wagonjwa kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mwanza na nje ya mkoa huo, hatua inayoweza kuchochea maendeleo ya sekta ya afya na utalii katika Kisiwa cha Ukerewe.

Amesema mazingira ya kisiwa hicho, pamoja na upatikanaji wa vyakula vya asili na mandhari yake, yanaweza kuongeza mvuto kwa watu wanaofika kwa ajili ya matibabu na mapumziko.

Ametoa wito kwa viongozi wa mkoa na wilaya kuangalia uwezekano wa kukiendeleza Ukerewe kuwa kitovu cha utalii katika Kanda ya Ziwa kwa kuimarisha vivutio vya utalii, fukwe na miundombinu ya usafiri.

Pia Makonda amependekeza kujengwa kwa eneo maalumu la kutua ndege za wagonjwa ili kurahisisha usafirishaji wa wagonjwa wanaohitaji matibabu ya haraka katika hospitali kubwa, ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Bugando.

Pia, ameomba kutengwa kwa eneo maalumu la mazoezi ya viungo kwa wagonjwa ili kusaidia mahitaji yao wakati wa matibabu na kuimarisha huduma zinazotolewa hospitalini hapo.

Waziri Makonda amesema ameridhishwa na miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa wilayani Ukerewe, ikiwemo ujenzi wa shule mpya, majengo ya halmashauri na miundombinu ya barabara.