Mtu mmoja ameuawa na wengine wasiopungua watano kujeruhiwa kufuatia shambulio la usiku kucha lililolenga vituo viwili vya mafuta mjini St Petersburg, Urusi.

Gavana wa eneo hilo, Alexander Beglov, amesema vikosi vya zimamoto vilikuwa vinapambana na moto uliotokea katika Kituo cha Mafuta cha St Petersburg na bohari ya mafuta ya Ruchyi baada ya mashambulizi hayo.

Kituo cha usafirishaji cha kampuni ya Ozon, inayofahamika kama "Amazon ya Urusi", pamoja na kituo cha data kinachomilikiwa na VKontakte (VK), mtandao wa kijamii unaofanana na Facebook nchini Urusi, pia viliripotiwa kushambuliwa.

Hadi sasa, Ukraine haijatoa tamko kuhusu mashambulizi hayo. Hata hivyo, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema Jumamosi kuwa Urusi imeilenga sekta ya nishati ya nchi yake mara 76 tangu Rais wa Marekani Donald Trump atangaze wiki iliyopita kile alichokiita "usitishaji wa mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati".

Ukraine ilikuwa imesitisha mashambulizi yake dhidi ya miundombinu ya mafuta ya Urusi kwa muda wa siku tatu baada ya tangazo hilo. Kyiv imekuwa ikisema mashambulizi hayo yanalenga kupunguza chanzo kikuu cha mapato kinachofadhili juhudi za vita za Moscow, huku ikiishutumu Urusi kwa kuendelea na mashambulizi yake wakati wa usitishaji huo.

Baadaye, Ukraine ilianza tena mashambulizi yake mapema wiki hii, hatua iliyomkasirisha Trump ambaye alitaka kuwe na makubaliano ya kusitisha mapigano ili kuwezesha utekelezaji wa makubaliano aliyofikia na Rais wa Urusi Vladimir Putin kuhusu usambazaji wa dizeli.

Ingawa Ukraine imewahi kuishambulia St Petersburg hapo awali, maeneo yaliyo karibu zaidi na mpaka wa Ukraine ndiyo ambayo kwa kawaida hukumbwa na mashambulizi mara nyingi zaidi. Kituo cha Mafuta cha St Petersburg kilishambuliwa mara ya mwisho mwezi Julai.

Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema ilidungua zaidi ya ndege zisizo na rubani 1,000 za Ukraine katika anga ya Urusi katika usiku wa kuamkia Jumapili.