
ARUSHA: WAFANYABIASHARA mkoani Arusha wametakiwa kuhakikisha vifaa vya kupimia wanavyotumia katika shughuli zao vinakaguliwa na kuthibitishwa na Wakala wa Vipimo (WMA) ili kuepuka hasara, migogoro na hatua za kisheria zinazoweza kujitokeza kutokana na matumizi ya vipimo visivyo sahihi.
Meneja wa WMA mkoani humo, Dismas Maturini, ametoa wito huo wakati wa ukaguzi wa kituo cha mafuta jijini Arusha, akisema vifaa vya kupimia vilivyo katika hali nzuri na vinavyotoa vipimo sahihi ni muhimu katika kulinda maslahi ya wafanyabiashara na walaji.
Amesema matumizi ya vifaa vyenye hitilafu, ikiwemo pampu za mafuta zinazovuja, yanaweza kusababisha hasara kwa mfanyabiashara na mteja, pamoja na kuchochea migogoro na kuwafanya wahusika kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

“Wafanyabiashara wanapaswa kuhakikisha vifaa vyao vya kupimia vinakaguliwa na kuthibitishwa kuwa vinakidhi viwango vinavyotakiwa kabla ya kuvitumia katika shughuli za biashara,” amesema Maturini.
Amesema ukaguzi wa vifaa hivyo ni sehemu muhimu ya kuhakikisha vipimo vinavyotolewa kwa wananchi ni sahihi na kwamba biashara zinafanyika kwa kuzingatia matakwa ya sheria.
Kwa upande wake, Ofisa Vipimo Mwandamizi mkoani humo, Jason Theonest, amesema wafanyabiashara wanapaswa kutumia huduma za WMA katika uhakiki wa vifaa vya vipimo ili kuhakikisha vinafanya kazi kwa usahihi na kukidhi matakwa ya kisheria.

“Ni muhimu mfanyabiashara kuhakikisha kifaa chake kimehakikiwa kabla ya kuanza kukitumia kibiashara, kwa sababu hatua hiyo inasaidia kuzingatia matakwa ya kisheria,” amesema Theonest.
Amesema wananchi nao wana nafasi muhimu katika kuhakikisha wanapata huduma kwa vipimo sahihi, akiwataka kuwa makini na kuangalia alama za uthibitisho wa ukaguzi kwenye vifaa vinavyotumika wakati wa kutoa huduma.
Kwa mujibu wa WMA, mita za maji zinaweza kuwa na muhuri maalumu (seal) unaoonyesha hali ya uthibitisho wa kifaa, huku pampu za mafuta na mizani inayotumika madukani, mabuchani na maeneo mengine ya biashara ikiwa na stika za uthibitisho wa ukaguzi kulingana na taratibu za Wakala huo.
Ukaguzi huo unalenga kuhakikisha vifaa vya kupimia vinakidhi viwango vinavyotakiwa na kutoa vipimo sahihi, hatua ambayo pia inalenga kulinda haki za walaji na wafanyabiashara.

Akizungumzia umuhimu wa ukaguzi huo, mfanyabiashara Grace Peter amesema ushirikiano na WMA unawasaidia wafanyabiashara kubaini mapema changamoto zinazoweza kujitokeza katika vifaa vyao na kuzitatua kabla hazijasababisha hasara.
Grace, ambaye alipeleka mzani wake katika ofisi za WMA mkoani Arusha kwa ajili ya ukaguzi, amesema alibaini kuwa mzani aliokuwa akiutumia katika biashara ulikuwa ukiongeza zaidi ya gramu 400, hali iliyokuwa ikimsababishia hasara.
“Ukaguzi huu unatupa fursa ya kubaini changamoto za vifaa vyetu na kuzirekebisha ili kuendelea kutoa huduma kwa wateja kwa usahihi,” amesema Grace.
Naye mfanyabiashara Rajabu Mohamed amesema uhakiki wa vipimo ni muhimu katika kujenga uaminifu kati ya wafanyabiashara na wateja, pamoja na kupunguza migogoro inayoweza kusababishwa na matumizi ya vipimo visivyo sahihi.
“Tunapohakikisha vifaa vyetu vinapima kwa usahihi, tunasaidia kujenga imani kwa wateja na kupunguza migogoro inayoweza kujitokeza katika biashara,” amesema Rajabu.
Akihitimisha, Maturini amewataka wananchi kuwa makini wanapopata huduma zinazohusisha vipimo na kutoa taarifa kwa WMA wanapobaini viashiria vya udanganyifu au matumizi ya vifaa visivyo sahihi.
“Tunawaasa wananchi kuwa makini na kuangalia alama za uthibitisho wa ukaguzi kwenye mita za maji, pampu za mafuta na mizani wanapotumia huduma mbalimbali. Wanapohisi kuna udanganyifu au vipimo visivyo sahihi, watoe taarifa kwa Wakala wa Vipimo ili hatua stahiki zichukuliwe,” amesema Maturini.
Wakala wa Vipimo unaendelea na jukumu la kuhakikisha vifaa vya kupimia vinavyotumika katika shughuli za kibiashara vinakidhi viwango vinavyotakiwa, kwa lengo la kulinda haki za walaji, wafanyabiashara na kuimarisha uadilifu katika biashara.
0 Comments