Wahamiaji wasiopungua 109, wakiwemo watoto 15, wamefariki dunia huku wengine 116 wakiripotiwa kupotea baada ya boti iliyokuwa imebeba watu 350 kuzama katika pwani ya Djibouti wakielekea Yemen, Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM) limesema.
Tukio hilo lilitokea usiku wa Oktoba 8 hadi 9 kaskazini mwa mji wa Obock, Djibouti, baada ya boti hiyo kupinduka ikiwa njiani kuvuka Mlango-Bahari wa Bab el-Mandeb kuelekea Yemen.
Kwa mujibu wa taarifa ya IOM iliyotolewa Jumapili, Oktoba 11, zaidi ya watu 80 walinusurika katika ajali hiyo. Wote walionusurika ni raia wa Ethiopia, ambao walikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakisafiri kwa boti hiyo.
Miongoni mwa miili 109 iliyopatikana ni ya wanaume 52, wanawake 42 na watoto 15, wakiwemo wasichana tisa na wavulana sita. Timu za IOM zinafanya kazi pamoja na mamlaka za Djibouti kutoa msaada wa dharura kwa manusura.
Mkuu wa IOM nchini Djibouti, Alexandre Coissac, amesema tukio hilo ni pigo kubwa na kueleza kuwa shirika hilo linawapa pole manusura pamoja na familia zilizopoteza wapendwa wao au ambazo bado hazijapata taarifa za ndugu zao.
IOM imesema umaskini, ukosefu wa usalama na athari zinazoongezeka za mabadiliko ya tabianchi ni miongoni mwa sababu zinazowasukuma wahamiaji kuhatarisha maisha yao katika safari hiyo, wakitafuta fursa za kiuchumi katika nchi za Ghuba kupitia Yemen, licha ya kuongezeka kwa machafuko huko Mashariki ya Kati.

0 Comments