Christa Pike, raia wa Marekani aliyenusurika jaribio la kunyongwa kwa sindano ya sumu, ameruhusiwa kutoka hospitalini na kurejeshwa gerezani siku 10 baada ya zoezi hilo lililofeli, kwa mujibu wa taarifa ya mawakili wake.

Pike, mwenye umri wa miaka 50, alidungwa sindano ya dawa ya pentobarbital mara mbili Septemba 30, katika jaribio la kutekeleza hukumu yake ya kifo katika jimbo la Tennessee. Zoezi hilo lilimuacha katika hali mahututi.

Mawakili wake wamesema Pike amerejea katika gereza alilokuwa akishikiliwa kwa takribani miaka 30 na ataendelea kupata huduma za matibabu. Hata hivyo, haijafahamika ni matibabu gani anayoendelea kupatiwa gerezani.

Pike alipata fahamu Jumanne na kuanza kuzungumza tena, jambo lililowashangaza wataalamu wa afya na mawakili wake. Wakili wake, Randy Spivey, amesema maneno yake ya kwanza yalikuwa, “Niko wapi?” na “Wewe ni nani?”

Kwa mujibu wa mawakili wake, Pike alikuwa na matatizo ya kiafya yaliyohusisha nimonia na kuvimba kwa mikono. Pia alisema alikuwa na hasira na kuchanganyikiwa, huku athari za muda mrefu za tukio hilo zikiwa bado hazijafahamika.

Pike alihukumiwa kifo kwa kushiriki katika mateso na mauaji ya Colleen Slemmer, mwenye umri wa miaka 19, mwaka 1995, akiwa na aliyekuwa mpenzi wake, Tadaryl Shipp. Mawakili wake sasa wanataka hukumu hiyo ibadilishwe kuwa kifungo cha maisha. Hadi sasa, mamlaka za Tennessee hazijaeleza kwa nini jaribio la kutekeleza hukumu hiyo lilishindwa na kama zitajaribu tena kumnyonga.