Watu 22 wamefariki na wengine kadhaa kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha basi na lori kwenye barabara kuu ya Nairobi-Mombasa nchini Kenya leo asubuhi.
Ajali hiyo inaripotiwa kutokea majira ya saa moja asubuhi, ambapo basi hilo lilikuwa limebeba abiria waliokuwa wakirejea kutoka kwenye shughuli ya mazishi wakati lilipogongana na lori hilo.
Waliojeruhiwa walikimbizwa katika hospitali ya Kaunti Ndogo ya Mtito Andei, ambapo wanapokea matibabu, huku miili ya waliofariki katika ajali hiyo ikihifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo.
Kamishna wa Kaunti ya Makueni ambako ajali hiyo ilitokea, Abdullahi Khalif, awali alikuwa amethibitisha vifo vya watu 20, kabla ya idadi hiyo kupanda na kufikia 22.

0 Comments