Serikali imeendelea kufungua milango kwa wawekezaji katika sekta ya madini baada ya Wizara ya Madini kutoa leseni tisa za utafiti wa madini kwa kampuni ya Saudi Gold Refinery kutoka Saudi Arabia, hatua inayotarajiwa kuchochea uwekezaji, kuongeza shughuli za utafiti na kufungua fursa mpya za uchimbaji nchini.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amesema utoaji wa leseni hizo umetokana na nia ya kampuni hiyo kuwekeza nchini, kufuatia mkutano wa kibiashara kati ya Tanzania na Saudi Arabia uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Mavunde amesema katika mkutano huo, Saudi Gold Refinery ilionesha dhamira ya kuwekeza katika sekta ya madini, ambapo Serikali iliahidi kuwezesha upatikanaji wa leseni za awali ndani ya siku saba za kazi. Amesema ahadi hiyo imetekelezwa na kampuni hiyo imeendelea kuomba maeneo mengine ya kufanya utafiti kupitia Tume ya Madini.

“Tuliwahakikishia wawekezaji hawa kwamba watapata leseni zao za awali ndani ya siku saba za kazi, na tumetekeleza ahadi hiyo. Baada ya hapo wameendelea kuomba maeneo mengine ya utafiti kupitia Tume ya Madini,” amesema Mavunde.

Amesema Serikali imeamua kutoa fursa hiyo kwa kampuni hiyo kutokana na uwezo wake wa kifedha, teknolojia na utaalamu wa kufanya utafiti wa kina wa madini, sambamba na rekodi yake ya uwekezaji katika maeneo mbalimbali.

Waziri Mavunde amesema Serikali pia inaendelea kupitia leseni za madini ambazo zimekuwa zikishikiliwa bila kufanyiwa kazi, akisisitiza kuwa maeneo yasiyotumika yatafutwa leseni na kutolewa kwa wawekezaji wenye uwezo na dhamira ya kuyaletea maendeleo.

“Serikali haitaruhusu mwekezaji kushikilia eneo kubwa bila kulifanyia kazi. Tunataka wawekezaji wenye dhamira ya kweli ya kufanya utafiti na baadaye kuanzisha shughuli za uchimbaji,” amesema.

Ameongeza kuwa baadhi ya maeneo yatakayorejeshwa Serikalini yatafungua fursa kwa wawekezaji wengine pamoja na wachimbaji wadogo kupitia programu ya Mining for Brighter Tomorrow, inayolenga kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika sekta ya madini.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Saudi Gold Refinery, Faisal Suleiman Aloithaim Mallim, amesema kampuni hiyo imepanga kuwekeza hadi dola milioni 10 za Marekani katika hatua za awali za utafiti wa madini nchini Tanzania, kwa lengo la kutathmini uwezo wa maeneo waliyopewa leseni na kubaini fursa zaidi za uchimbaji.

Amesema uwekezaji huo utaanzia katika shughuli za utafiti na kuendelea hadi hatua ya upembuzi yakinifu, hatua ambayo inaweza kufungua milango ya uwekezaji mkubwa na wa muda mrefu katika sekta ya madini nchini.

Mallim amesema kampuni hiyo imejipanga kutumia nguvu kazi ya Watanzania, pamoja na bidhaa na huduma zinazopatikana nchini, huku ikishirikiana na kampuni za ndani ili kuhakikisha uwekezaji wake unaleta manufaa mapana kwa uchumi wa Tanzania.

“Tunapoingia katika nchi mpya, ni muhimu kuunga mkono uchumi wa nchi hiyo. Watu wa ndani wanapaswa kunufaika na biashara yetu; si kuingia na kuondoka bila kutoa manufaa kwa wenyeji,” amesema.

Kwa mujibu wa Mavunde, utoaji wa leseni hizo tisa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuvutia mitaji yenye tija katika sekta ya madini, kuongeza ajira na shughuli za kiuchumi, sambamba na kuimarisha mchango wa sekta hiyo katika mapato na maendeleo ya Taifa.