Kuimarika kwa uzalishaji wa bidhaa nchini kunatarajiwa kuwa miongoni mwa nguzo muhimu za kukuza uchumi jumuishi, kupanua fursa za ajira na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi, kupitia utekelezaji wa sera mpya ya Maendeleo Endelevu ya viwanda na sera ujasiriamali Ndogo na za kati ya mwaka 2003 Toleo la mwaka 2025.
Akizungumza na Waandishi wa habari Jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Uhandisi na Usanifu Mitambo Tanzania (TEMDO) Eng. Profesa Frederick C. Kahimba, amesema sera hizo zimeweka msingi wa kuimarisha uwezo wa viwanda vya ndani kuchakata malighafi zinazopatikana nchini na kuzibadilisha kuwa bidhaa zenye thamani hatua itakayosaidia kuongeza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa taifa.
Akizungumza mara baada ya hafla ya uzinduzi wa sera hizo, Kahimba amesema maendeleo ya viwanda yana nafasi kubwa katika kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira, akitoa mfano wa viwanda vikubwa vya nguo ambavyo vina uwezo wa kuajiri maelfu ya Watanzania na kuchochea shughuli nyingine za kiuchumi.
Amesema kuongeza uzalishaji wa bidhaa zinazotengenezwa nchini kutasaidia kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje, kulinda ajira za ndani na kupunguza matumizi ya fedha za kigeni, huku uzalishaji wa ziada ukifungua fursa za kuuza bidhaa za Tanzania katika masoko ya kimataifa.
Akifafanua mchango wa taasisi anayoiwakilisha katika kukuza sekta hiyo, Kahimba amesema ina majukumu ya kufanya tafiti za teknolojia za viwandani, kutoa huduma za kihandisi kwa viwanda, kuandaa mafunzo ya kitaalamu na kubuni teknolojia zinazoongeza thamani ya mazao na bidhaa mbalimbali.
Ameeleza kuwa teknolojia hizo zinahusisha sekta za kilimo, mifugo, madini na afya, kwa lengo la kuongeza tija na kujenga uwezo wa kutumia rasilimali zilizopo nchini kuzalisha bidhaa zenye thamani zaidi.
Aidha, amewahimiza Watanzania kuunga mkono bidhaa zinazozalishwa nchini kwa kuzitumia na kuziamini, akisisitiza kuwa mafanikio ya sera hizo yanahitaji ushirikiano wa Serikali, sekta binafsi, wajasiriamali na wananchi katika kujenga viwanda imara vitakavyopanua ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Taasisi ya Uhandisi na Usanifu Mitambo Tanzania (TEMDO) inabuni na kutengeneza mashine mbalimbali za kusaidia uzalishaji na kuongeza thamani ya malighafi, miongoni mwa mashine hizo ni za kukamua mafuta ya alizeti, kusindika matunda, kupukuchua mahindi, kusindika maziwa na asali, kutengeneza chakula cha mifugo na kuchakata ngozi, pia hutengeneza vifaa tiba kama vitanda vya wagonjwa, kwa lengo la kupunguza gharama za uzalishaji na kukuza viwanda vya ndani.
.jpeg)


0 Comments