Mke wa Balozi wa Marekani nchini, Jackie Lenhardt, amewataka yatima na watoto wanaoishi katika mazingira magumu kujenga utamaduni wa kusoma magazeti, kusikiliza redio na kuangalia televisheni kila wanapopata nafasi ili kujifunza mambo mapya ya kijamii na kujiongezea uelewa.
Aidha, Jackie amesema kutokana na mazingira magumu yanayowakabili amewaomba watoto hao kutokata tamaa na kwamba maisha wanaoyoishi yanaweza kubadilika wakati wowote kulingana na mahitaji ya wakati.
Alitoa changamoto hiyo juzi alipotembelea kituo cha kulelea watoto cha Kiwohede na kuzungumza nao kabla ya kula nao chakula cha mchana.( Pichani Balozi wa Marekani Tanzania bwana Alfonso na mkewe bibi Jackie).
Alisema uyatima usiwaodolee haki ya kupata habari hasa za kijamii na kusisitiza kupata habari kunaweza kuwaongezea uelewa na fursa ya kujua mengi yanayohusu maisha na maendeleo ya mtu mmoja mmoja bila kujali ni yatima au la.
"Watu hasa watoto wanaopata nafasi ya kusoma, kusikiliza na kuangalia vipindi vizuri vya televisheni uwezo wao wa kujua na kutambua mambo huwa unaongezeka kulinganisha na wale wasiojua chochote," alisema.
Jackie amejiwekea utaratibu wa kutembelea kituo hicho kila Alahamisi ili kufanyakazi za watoto na kuzungumza nao hatua ambayo anaamini inaweza kuamsha ari na kuwaondolea dhana kuwa hawathaminiwi.
Mapema akizungumza katika halfa hiyo, afisa mradi wa Kiwohede, Stalla Mwambenja alisema moja kati ya majukumu ya asasi hiyo ni kuwatafutia watoto wafadhili ili wasaidie maisha ya kila siku ikiwemo elimu ya ufundi.
Alisema Jackie ni mmoja kati ya wafadhili wanaosaidia kwa hali na mali maisha ya watoto wanaolelewa katika kituo hicho kinachowalenga watoto wenye umri kati ya miaka tisa hadi 25 ili kuwajengea uwezo hatimaye wawe na uwezo wa kujitegemea.
Mmoja wa watoto hao, Shukuru Kidoga (17) alisema ujio wa Jackie na marafiki zake kituoni hapo umewapa faraja na kuwataka watu wengine wenye huruma kujitokeza ili kusaidiana na viongozi wa Kihowede katika kusaidia watu wa makundi maalum kama wao.