Mufti wa Tanzania, Sheikh Mkuu, Issa bin Shaaban Simba, amesema wameiandikia serikali barua kuomba siku ya Mwaka Mpya wa Kiislamu kuwamo katika orodha ya sikukuu zinazotambuliwa kuwa ni siku rasmi za mapumziko ya kitaifa nchini.
Alisema hayo wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari katika mkutano wa wanahabari aliouitisha makao makuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) jana kwa lengo la kutoa salaamu za mwaka mpya wa Kiislamu wa 1432, maarufu kama Alhjriyyah (A.H.).
Mufti Simba alisema wamefikia hatua hiyo ili kurekebisha makosa yaliyofanywa na viongozi wa Kiislamu waliopita kuhusu Sikukuu za Kiislamu, ambazo zinapaswa kuwa siku rasmi za mapumziko kitaifa.
Alisema viongozi hao walipotakiwa na serikali kuorodhesha sikukuu hizo, walitaja kuwa ni tatu; ambazo ni Iddi-El-Fitr, Idd-El-Hajj na Maulid na kuacha kuorodhesha Mwaka Mpya wa Kiislamu.
Hivyo, kwa kuliona hilo, tumeiandikia barua serikali kuomba Mwaka Mpya wa Kiislamu uwe pia siku ya mapumziko. Tunasubiri majibu kutoka serikalini,” alisema.
Mufti Simba mbali ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwafikisha katika mwaka huo aliwataka Waislamu kuelekeza fikra zao katika mwaka uliopita kwa kutaza waliyofanya katika kujenga maendeleo yao, kiimani katika familia na jamii yao kama Waislamu.
Alisema wanaposherehekea kumalizika kwa mwaka 1431 na kuingia mwaka 1432, wanapaswa kuzingatia maana ya neno “Hijria”, ambayo alisema inamaanisha ‘kuhama’ Mtume Muhammad (S.A.W.) kutoka Makka kwenda Madina kama alivyoamrishwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kuinusuru dini.
Aliwataka Waislamu kutoipoteza maana hiyo katika fikra na nyoyo zao, badala yake wawajibike kufanya ‘Hijra’ kwa maana kuyahama maovu na kuelekea kwenye mema.
Alisema katika kujenga ufanisi katika maisha ya Waislamu, Mwenyezi Mungu amewaamrisha kujenga umoja na mshikamano, kujitolea mali zao na nafsi zao katika njia ya Mungu, pia kujielimisha na kuukimbia ujinga, kuamrisha mema na kukataza mabaya.
Alimuomba Mwenyezi Mungu awape mafanikio Waislamu na wananchi wa Tanzania kwa jumla na kumbariki Rais Jakaya Kikwete pamoja na Baraza lake la Mawaziri walifanyie Hijra taifa lihame kutoka Watanzania walipo na kuelekea kwenye mafanikio zaidi.