Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imepokea risiti ya kununulia pingu anazodaiwa kukutwa nazo Mtangazaji wa Shirika la Habari Tanzania (TBC1), Jerry Muro, alipokamatwa na polisi.
Risiti hiyo yenye namba 341573B, ilitolewa jana na Shahidi Anthony Mwita (45), mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Gabriel Mirumbe, anayesikiliza kesi hiyo ya kuomba rushwa ya Sh. milioni 10, inayomkabili Muro na wenzake.
Shahidi huyo ambaye ni Mpelelezi, aliieleza mahakama kuwa, aliipata risiti hiyo katika duka la silaha la Mzinga linalomilikiwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), lililopo Upanga, jijini Dar es Salaam.
Nilikwenda dukani hapo kupata uthibitisho kama mshtakiwa alinunua pingu hiyo dukani hapo na walinithibitishia kumuuzia pingu hiyo yenye thamani ya Sh.25, 000, Mei 26, mwaka 2009” alieleza.
Baada ya maelezo hayo ya shahidi, mahakama ilipokea risiti hiyo kama kielezo katika kesi hiyo.
Pia, shahidi huyo alieleza kuwa, katika upelelezi wake alienda katika hoteli ya Seacliff, ili kuthibitisha kama Muro alifika hotelini hapo Januari 29, mwaka 2010, ambapo ilionyesha kwenye orodha ya daftari la magari yaliyoingia, gari la mshtakiwa huyo lenye namba T 545 aina ya Cresta iliingia saa 7:33 mchana na kuondoka saa 8:44 mchana.
Mwita aliendele kueleza kuwa, pia aliuomba uongozi wa hoteli hiyo kuonyeshwa picha katika kamera ya CCTV ya matukio ya Januari 29, mwaka jana, ambapo alionyeshwa na kupatiwa nakala ya picha hizo, lengo likiwa ni kuthibitisha kama kweli
Muro alifika hotelini siku hiyo.
Wakati huohuo, shahidi wa nne, Mpelelezi Issa Seleman, alidai kuwa, baada ya mlalamikaji Michael Wage, kuombwa rushwa na mshitakiwa huyo, alikwenda kutoa taarifa polisi juu ya suala hilo.
Alidai kuwa, mshtakiwa alimtaka mlalamikaji wakutane katika geti la ofisi za TBC1 ili akabidhiwe Sh. milioni 10.
Hata hivyo, shahidi huyo alieleza kuwa, mlalamikaji kwa kushirikiana na polisi walimtaka mshitakiwa wakutane katika mgahawa wa City Garden, ambako walikuwa wameweka mtego wa kumkamata.
Siku tulipoweka mtego, Muro alifika baada ya kama dakika tano hivi na kumpigia simu Wage kumfahamisha ameshafika, Muro akamuonyeshea Wage ishara ya kumuita naye akamfuata, wakati anaingia ndani ya gari mguu mmoja ukiwa nje, Muro alihisi kama kuna mtego amewekewa na kumfukuza Wage ashuke kwenye gari yake,” alidai shahidi huyo.
Alieleza kuwa, walimfuata Muro na kumuuliza kama anamfahamu Wage, lakini alikana kumfahamu, akieleza kuwa alifika eneo hilo kufuatilia habari ya China.
Alisema pamoja na maelezo hayo ya mshitakiwa, askari hao walimuomba kufika kituoni kwa maelezo zaidi.
Kesi hiyo itaendelea tena leo.