WADAU wa maendeleo nchini wameishauri Serikali ipunguze malipo ya mishahara na posho za wabunge na fedha zitokanazo na punguzo hilo, ziongezwe kwenye mishahara ya wataalamu wa fani mbalimbali. Kwa mujibu wa wadau hao, hilo likitekelezwa litakuwa suluhisho la kupotea kwa wataalamu wanaokimbilia siasa kwa madai ya kutafuta maslahi bora. Wakizungumza jana katika mjadala wa mapitio ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025 jana, wadau hao pia walipendekeza kufutwa kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU), kwa madai imeshindwa kukomesha rushwa ambayo walisema ndio chanzo cha maisha magumu ya Watanzania.

Wadau hao waliokutana katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi ya Utafiti wa Masuala ya Uchumi na Jamii (ESRF) Dar es Salaam walisema si sahihi wala haki kuwalipa wabunge mishahara mikubwa zaidi ya wataalamu, kwa kuwa wao si watendaji wa moja kwa moja.

Majadiliano hayo yaliongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa ESRF, Dk. Hoseana Lunogelo, anayeongoza timu ya watafiti tisa waliochaguliwa na Tume ya Mipango kukusanya maoni ya wananchi kuhusu dira hiyo kwa ajili ya kuiboresha, kwa matumizi ya miaka 15 iliyobaki.

Wadau hao, waliosisitiza kutoandikwa majina yao gazetini, bali waitwe wadau, walikuwa wakichangia mawazo kuhusu nini kiongezwe au kipunguzwe katika Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025 iliyoanza kutekelezwa mwaka 2000.

Katika mjadala huo waliafikiana kuwa ili maendeleo yaliyoainishwa kwenye dira hiyo yafikiwe, Serikali haina budi kuondoa tofauti kubwa ya mishahara inayolipwa kati ya wataalamu na wabunge (wanasiasa).

“Si kuondoa tofauti kubwa ya malipo ya mishahara na posho tu, bali kuishusha nyanja ya siasa kutoka nafasi ya kwanza ya kimaslahi iliyopo sasa na kuwa ya pili, baada ya taaluma.

“Hili linawezekana kama wanasiasa wenyewe watafahamu umuhimu wa wataalamu na kukubali kuacha ubinafsi wa kimaslahi walionao,” alisema mmoja wa wadau waliochangia mada hiyo.

Mdau wa pili alifafanua kuwa siasa ya Tanzania imekuwa lulu kiasi cha wataalamu wa afya kuacha wagonjwa hospitalini na kuvamia majukwaa ya siasa huku walimu wakikimbia chaki na kwenda mitaani kuelimisha watu namna ya kupokea hongo ili kuwachagua.

“Wataalamu wanakimbia kazi zao, walindwe hawa wasipotee, nchi haiwezi kusimama imara bila wao, ifanyike namna wasitoroke fani na kukimbilia ubunge, wanachokifuata kule ni maslahi binafsi, Serikali iyapunguze tuone kama hawatabaki kwenye taaluma zao,” alishauri mdau mwingine.

Kadhalika, ilipendekezwa kuwepo na utaratibu utakaowafanya watu binafsi waikimbie siasa na kuhamia kwenye shughuli nyingine za maendeleo, mfano kilimo, kwa maelezo kuwa kimetelekezwa kivitendo na kubaki kubadilishiwa kaulimbiu kila kukicha bila kuleta mafanikio dhahiri yanayotarajiwa.

“Kilianza kuitwa Uti wa Mgongo, baadaye kikaitwa Msingi wa Maisha na sasa ni Kilimo Kwanza … hizi ni kaulimbiu za wanasiasa, sasa tunawataka hao hao warudi kukitekeleza kwa vitendo, ili kimnufaishe mwananchi, maslahi yao yakipunguzwa watakithamini kilimo kwa vitendo, hili linawezekana,” alisema mchangiaji mwingine.

Wakifafanua sababu za kufutwa kwa Takukuru walisema hawaoni kazi yake kwa kuwa inalinda maslahi ya wachache na kusahau kuwa wananchi ndio wanaoteswa na rushwa.

Walisema, rushwa imechangia kuporomoka kwa maadili ya viongozi wengi nchini na imewafanya wasionacho kukosa huduma wanazostahili huku mgawanyo wa kila kitu kuanzia ardhi na madaraka ukinufaisha wenyenacho.

“Afadhali misingi ya Azimio la Arusha irejeshwe, pengine maadili ya viongozi yatazingatiwa,” alisema mchangiaji mwingine.