Mamia kwa maelfu ya watu walitazamiwa kushiriki maandamano makubwa katikati ya mji mkuu wa Yemen, Sanaa wiki moja baada ya watu hamsini kuuawa na vikosi vya usalama wakati wakiandamana.
Waandamanaji walikuwa wamepanga maandamano makubwa kuwahi kufanyika ya kudai Rais Ali Abdullah Saleh ajiuzulu.

Bw Saleh ameuambia mkutano wa halaiki ya wafuasi wake kuwa yuko tayari kuachia madaraka, ila tu kwa mtu anayemuamini.
Askari walifyatua risasi angani kuwazuia wafuasi wa Bw Saleh wasielekee waliko waandamanaji wanaompinga kiongozi wao.
Katika hotuba yake, Rais Saleh ambaye amekuwa madarakani kwa zaidi ya miongo mitatu ameshutumu mauaji ingawa aliwataka wafuasi wake wawe na msimamo imara.
Kabla ya hotuba hiyo alikanusha kuwa alihusika kwa vyovyote vile katika mauaji ya waandamanaji wiki iliyopita.
Shirika la Amnesty International limeionya serikali dhidi ya matumizi ya nguvu ya kupindukia, na kuongezea kuwa serikali haiwezi kutumia risasi kutanzua mgogoro unaoikabili.