MAHAKAMA ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) jana ilimhukumu Meya wa zamani wa Rwanda, Gregoire Ndahimana kifungo cha miaka 15 jela baada ya kumtia hatiani kwa makosa mawili ya mauaji ya kimbari na kuteketeza kizazi kama uhalifu dhidi ya binadamu.

“Majaji wawili kati ya jopo la majaji watu wamekubaliana kumhukumu Ndahimana adhabu moja ya kifungo cha miaka 15 jela,” Jaji Kiongozi Florence Rita Arrey alitamka huku akiwa amezungukwa na majaji wenzake, Bakhtiyar Tuzmukhamedov na Aydin Sefa Akay.

Ndahimana mwenye umri wa miaka 59, alikuwa Meya wa Wilaya ya Kivumu, Mkoa wa Kibuye, Magharibi ya Rwanda, pamoja na mambo mengine anadaiwa kushirikiana na viongozi wengine wilayani humo kufanya mauaji dhidi ya Watusti waliokuwa wanapata hifadhi ya maisha yao ndani ya Kanisa la Nyange, kati ya Aprili 14 na 16, 1994.

Hukumu imefafanua kwamba, Ndahimana amepatikana na hatia katika kosa la mauaji ya kimbari na kuteketeza kizazi kwa kuunga mkono kutendeka kwa mauaji hayo kwa kutumia mamlaka yake dhidi ya polisi waliokuwa chini ya himaya yake.

“Ndahimana alikuwa na mamlaka ya kuwadhibiti polisi wilayani mwake. Majaji wawili kati ya watatu, tumemtia hatiano kwa uhalifu huo kwa kushindwa kwake kuwaadhibu polisi wa wilaya yake kwa kushiriki mauaji katika Kanisa la Nyange Aprili 15, 1994,” ilifafanua mahakama katika hukumu yake.



Mahakama pia ilibaini kwamba kuwepo kwa Ndahimana siku ya kubomolewa kwa Kanisa la Nyange huku wakimbizi zaidi ya 2000 wakiwemo ndani yake, kulitoa hamasa kwa washambuliaji kwa sababu mtuhumiwa huyo alikuwa na madaraka ya umeya wa wilaya hiyo.

Katika maamuzi yake, pia mahakama umetupilia mbali madai mengi ya mwendesha mashitaka dhidi ya Ndahimana kwa kile ilichoelezwa kuwa “kushindwa kwa mwendesha mashitaka kuthibitisha tuhuma pasipo mashaka” ingawaje imebainika kuwa mshitakiwa alikuwepo katika baadhi ya mikutano ya kupanga na kuchochea mauaji ya kimbari pamoja na wakati wa kubomolewa kanisa la Nyange.

Wakili Kiongozi wa meya huyo wa zamani, Barat Chadha ameilezea hukumu hiyo kuwa “siyo mbaya” na kwamba ana matumaini kuwa mteja wake anaweza kuachiwa katika ngazi ya Mahakama ya Rufaa.

Naye Mwendesha Mashitaka wa ICTR, Hassan Bubacar Jallow aliwaambia waandishi wa habari katika taarifa yake fupi baada ya hukumu hiyo kuwa haridhiki nayo kwenye baadhi ya vipengele vilivyomwachia huru Ndahimana.

“Ofisi ya Mwendesha Mashitaka inatarajia kukata rufaa dhidi ya hukumu na adhabu iliyotolewa,” alisema Jallow.

Wengine waliokwishatiwa hatiani kwa mauaji yaliyofanyika katika kanisa hilo la Nyange ni Padri wa kanisa hilo, Athanase Seromba anayetumikia kifungo cha maisha jela na mfanyabiashara Gaspar Kanyarukiga aliyehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na anasubiri tarehe ya kusikilizwa rufaa yake kupinga adhabu hiyo.