Na Mwandishi Wetu
STAA wa filamu Bongo, Irene Uwoya amefunguka kuwa, kabla ya ndoa amewahi kufanya mapenzi bila kutumia kinga, kitendo ambacho amekijutia kwa asilimia 50 za mtazamo wake.

Mwanadada huyo aliwatia mshangao wa ‘aisee Uwoya’ baadhi ya wasikilizaji waliokuwa wamekikodolea macho na kukitegea masikio Kipindi cha Mikasi cha Salama Jabir kilichorushwa hewani hivi karibuni na Televisheni ya Channel 5.

ILIKUWAJE ASEME HIVYO?
Uwoya alijikuta akizibua moja ya koki ya matendo yake ya nyuma kabla ya kuolewa na msakata kabumbu Hamad Ndikumana ‘Kataut’ raia wa Rwanda, baada ya kutupiwa swali na mtangazaji wa kipindi hicho hivi: “Umeshawahi kufanya mapenzi bila kinga?”

Kabla hajajibu, staa huyo mwenye macho makubwa yenye mvuto alipepesa kope na kurembua macho kwanza kisha kuachia kibomu: “Yaa! Nimeshawahi kufanya, lakini kabla ya ndoa …” kicheko na aibu kwa mbali vilichukua nafasi kwa dakika chache baada ya jibu hilo.
 Akiwa kama mtu aliyeelemewa na uzito wa kile alichokitamka, msanii huyo aliongezea maneno yanayotafsirika kama kufukia bonde: “Ila ni mara moja tu…nina maana na mtu mmoja.”

KUMTAJA AY
Hata hivyo, wakati akihenya na swali la ngono zembe, Uwoya alijikuta akimtaja mwanamuziki nyota wa Bongo, Ambwene Yessaya ‘AY’ baada ya kutakiwa kutoa ufafanuzi wa kuwepo kwa madai kuwa yuko ‘vere klozi’ naye.

“AY ni mtu wangu wa karibu, nimefahamiana naye muda mrefu tangu alipokuwa Dodoma, unajua wazazi wetu ni marafiki,” alisema Uwoya huku akimtazama mtangazaji wa kipindi ambaye hata hivyo hakusita kumtwaga swali lingine fasta.

“Au ndo’ huyo uliyecheza naye bila kinga?” Aliulizwa na Salama, lakini weee, aliangua kicheko kilichowafanya washiriki wengine wa kipindi wazidi kusisitiza “atakuwa huyo” jambo lililomfanya Uwoya aseme, “...no, no, noo.”

Hata hivyo watazamaji wengi walilaani kauli hiyo ya Uwoya kwa madai kuwa, haikustahili kutolewa na mtu aliyeolewa kwa ajili ya heshima ya ndoa yake na hivyo kumshangaa staa huyo ambaye hivi karibuni alidaiwa kuachana na mumewe kisha kurudiana.