Na Musa Mateja
OHOOO! Siku chache baada ya ndoa ya Legendary wa Bongo Fleva, Judith Wambura Mbibo ‘Jide’ na mtangazaji mahiri nchini, Gardner Gabriel Habash ‘G Habash’ kudaiwa kuvunjika, gumzo limeibuka kufuatia kunaswa kwa picha za Jide na kijana mmoja (dogodogo) aliyetajwa kwa jina la Meddy Ahmed ‘Mtoto wa Vitoto’, Risasi Jumamosi linakupa kinaga ubaga.TUJIUNGE NA CHANZO
Kwa mujibu wa chanzo makini, Mtoto wa Vitoto huyo amekuwa na urafiki uliotukuka na Jide kwa muda mrefu kabla na baada ya mtafaruku wa ndoa ya Jide na mumewe Gardner hivyo kudaiwa kuwa ndiyo faraja ya mawazo ya mwanamuziki huyo hususan kipindi hiki cha changamoto ya mgogoro wa ndoa yake.
Chanzo hicho kilizidi kumwaga data kuwa, ukaribu wa Jide na bwa’mdogo huyo ulipitiliza kiasi cha watu wa karibu na staa huyo kuanza kuhisi huenda wana uhusiano usiofaa.
“Ukaribu wao ulipitiliza hadi kila mtu wa karibu na Jide akautilia shaka, isitoshe kama unavyojua, Jide si mtu wa kuweka mambo yake hadharani. Mbaya zaidi Jide amekuwa akimposti dogo huyo kwenye mitandao yake ya kijamii,” kilisema chanzo hicho.APEWA NAFASI YA TATU

Wakati paparazi wetu akiendelea kukusanya data kuhusiana na ishu hiyo, chanzo hicho kilizidi kushibisha maelezo yake kwa kusema Jide amekuwa akimwandika nambari tatu dogo huyo kwenye mitandao ya kijamii ambapo baadhi ya watu eti wanatafsiri kuwa, maana yake ni kwanza mumewe (Gardner), ya pili yeye (Jide) na ya tatu ni dogo huyo.
“Dogo yuko sawa na Jide maana ukitaka kuamini fuatilieni kwa ukaribu mtawaona tu hata katika mitoko ya Jaydee (Jide). Kuna picha kibao zipo kwenye akaunti yake, dogo anaonekana akiwa kwenye ndinga (gari) la Jide ingawa dogo yuko makini kweli na suala hilo, nafikiri wamewekeana mikakati ya kuwa wa siri,” kilisema chanzo hicho.PICHA ZATUA RISASI
Baada ya paparazi wetu kupewa mchongo huo, alianza kuzisaka picha hizo kupitia vyanzo vyake mbalimbali na kufanikiwa kuzidaka zikimuonesha bwa’mdogo huyo akijiachia juu ya ndinga inayodaiwa ni ya Jide katika pozi tofautitofauti.
Kama hiyo haitoshi, kupitia akaunti ya Jide ya Instagram, zilionekana picha tofauti za dogo huyo, ikiwemo ile ambayo aliiunganisha picha tatu tofauti, mbili za kwake na moja waliyokuwa ‘klozdi’ na Mtoto wa Vitoto.

JIDE ALIPOTAFUTWA!
Katika kutaka kujua ukweli wa ukaribu wa wawili hao na kufuatilia mwenendo mzima wa viwanja vyao vya starehe, paparazi wetu alimvutia waya Jide lakini simu yake haikupatikana hewani kwa siku tatu mfululizo.DOGODOGO SASA

Baada ya Jide kutopatikana hewani, Jumatano iliyopita paparazi wetu alimtwangia simu Mtoto wa Vitoto ili kumsikia anauzungumziaje ukaribu wake na sista huyo ambapo baada ya kusomewa mkasa mzima, dogo alikata simu kwa madai kuwa sehemu aliyokuwa siku hiyo haikuwa nzuri na kuahidi kumpigia paparazi wetu baadaye lakini hakufanya hivyo hadi kesho yake (Alhamisi) alipopigiwa tena na gazeti hili na kupokea.
ADAI NI MARAFIKI
Huku akiashiria sauti ya kutojiamini, dogo huyo alisema yeye na Jide ni marafiki wakubwa katika mazingira ya kawaida, pia  ni shabiki wake kama walivyo wengine ila ishu ya picha mtu yeyote anaweza kupiga.

Kuhusu kuendesha gari linalodaiwa ni la Jide, dogo alisema hajawahi ila ameshapiga nalo picha na mtu yeyote anaweza kufanya hivyo kama ana uhusiano mzuri na mwanamuziki huyo.
“Jide ni rafiki yangu na mimi ni shabiki wake wa kawaida. Kwa hiyo hilo siyo tatizo lakini pia kuhusu gari mimi sijawahi kuendesha gari la Jide lakini nimewahi kupiga nalo picha kweli kama shabiki mwingine na hakuna shida, ila siyo wapenzi, ni marafiki tu,” alisema Mtoto wa Vitoto.

ATUMA UJUMBE WA MASIHARA
Baada ya kuzungumza hayo, Mtoto wa Vitoto alikata simu na baada ya dakika tatu alituma ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) kwenye simu ya paparazi wetu uliosomeka hivi: “Acha kunizingua mwana.” 
Paparazi wetu alipompigia simu kwa mara nyingine kutaka kujua alikuwa na maana gani, dogo huyo hakupokea simu na hata alipoandikiwa SMS kwamba atoe ufafanuzi kuhusu ujumbe wake huo, hakujibu chochote hadi gazeti hili linakwenda mitamboni.

MTOTO WA VITOTO NI NANI?
Mtoto wa Vitoto ni kijana wa mjini tu, si Mbongo Fleva wala si Mbongo Muvi ila inadaiwa kwa sasa anafanya shughuli zake mkoani Morogoro. Amewahi kuishi Magomeni, Dar ambapo kwa sasa anadaiwa kuhamia Kinondoni, Dar. Ana asili ya Zanzibar.