Polisi nchini Mexico wamesema kiongozi wa genge moja la wauzaji mihadarati mjini Ciudad Juarez, anayezuiliwa na polisi amekiri kuidhinisha mauaji ya watu wengi katika eneo hilo mwaka mmoja uliopita.
Arturo Gallegos Castrellon alikamatwa mwishoni mwa wiki iliyopita pamoja na viongozi wengine wawili wanaoshukiwa kuwa wa genge lake.
Makao makuu ya polisi yamesema miongoni mwa mauaji aliyokiri ni pamoja na kupigwa risasi kwa mama mmoja mja mzito aliyekuwa akifanya kazi katika ubalozi wa Marekani mjini Ciudad Juarez na pia shambulio la sherehe moja lililosababisha vifo vya watu kumi na watano wengi wao wakiwa vijana.
Hata hivyo madai hayo ya Castrellon hayajathibitishwa rasmi.