Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, amesema shutuma zilizoelekezwa kwa chama hicho na mfanyabiashara wa Zanzibar, Mohamed Raza, kuwa chama hicho kimewatenga baadhi ya viongozi wastaafu wa Zanzibar hazina msingi na ni za uzushi.
Akizungumza jana, Makamba alisema kauli ya Raza kuwa CCM inawatenga baadhi ya viongozi wastaafu Zanzibar hasa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu ni upotoshaji mkubwa na wa makusudi.
Alisema viongozi hao walishirikishwa katika hatua zote za mikutano ya kampeni hivyo anamshangaa Raza kusema kuwa walitelekezwa.
habari zaidi....“Katika kampeni tulikuwa na aina mbili za mikutano, ile ya ndani na mikutano ya wazi na viongozi wastaafu walikuwa wakihudhuria mikutano hiyo sasa huyo Raza maneno kayatoa wapi,” alisema Makamba.
“Dk. Salmin Amour alihudhuria mkutano wa kufunga kampeni pale Kibandamaiti, amehudhuria mkutano wa NEC uliompitisha Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, “ alisema.
Raza alisema kama CCM haitajipanga vizuri inaweza kuishia mwaka 2015 kwani kuna mpasuko mkubwa visiwani humo.
Lakini Makamba alimjibu kuwa CCM itaendelea kuwa katika serikali ya Zanzibar kwa miaka yote hata kama itashindwa katika uchaguzi wowote.
“Katika mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar, chama kinachoshinda uchaguzi kinaunda serikali ya mseto hivyo hata kama CCM itashindwa itaendelea kuwemo serikalini, ina maana huyo Raza hajui mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar, Kama hajui aje tumfundishe,” alisema Makamba.
Kuhusu kauli kwamba mpasuko huo ndio umesababisha ushindi finyu wa CCM mwaka huu, Makamba alisema CCM haijawahi kushinda kwa kishindo Zanzibar hata uchaguzi mmoja.
Alisema miaka yote CCM imekuwa ikiishinda CUF kwa tofauti ndogo hivyo kauli ya Raza haina kitu kipya.
”Muulize Raza lini CCM iliwahi kushinda kwa ushindi mkubwa Zanzibar. Siku zote tunashinda kwa tofauti ndogo sana hivyo sielewi Raza anataka kusema nini,” alisema.
Raza alidai kuna matabaka yanayojengwa kati ya marais wastaafu na kuonya iwapo hali hiyo haitarekebishwa haraka, kuna hatari kwa CCM kufikia mwisho wake katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Raza aliyekuwa mshauri wa zamani wa masuala ya michezo wa Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour, alisema anatoa tahadhari hiyo akiwa ni mwanachama na kada mkereketwa wa CCM akizingatia Katiba na uwazi wa chama chake kuruhusu wanachama kutoa maoni yao kwa chama.
Alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.
Raza alisema matabaka kati ya marais wastaafu yalianza kudhihirika ilipoingia awamu ya sita, ambapo mmoja wa viongozi wastaafu Zanzibar alifuatwa nyumbani na kunyang’anywa magari.
“Akaondoshewa mpaka ulinzi, ile gari ya kuongoza. Akaachiwa kibaiskeli tu, lakini tukasema jamani tunakwenda kwenye amani. Kiongozi kanyang’anywa magari na mambo mengine mengi,” alisema.
Hata hivyo, alisema serikali ya awamu ya saba ilipoingia madarakani, kabla ya ile ya awamu ya sita kumaliza kipindi chake, ndani ya siku sita tu, mmoja wa viongozi wastaafu alipewa gari mpya aina Benz.
“Naomba sana CCM, vyombo vinavyohusika, wastaafu wote watendewe haki kulingana na taratibu. Au tuambiwe kama mstaafu huyu ana kadi ya CCM ‘A’ huyu mstaafu wa pili ana kadi ya CCM ‘B’, huyu mstaafu ana kadi ya CCM `C, lakini ninachojua mimi wastaafu wote ni sawa, hakuna mkubwa wala mdogo.
Alisema lazima kuwepo na usawa kwa viongozi wastaafu Zanzibar kwa kila mmoja kupata stahiki yake kwa mujibu wa taratibu ya katiba na sheria.
Pia aliwataka Watanzania kushukuru na kufurahia maridhiano yaliyofikiwa kati ya CCM na Chama cha Wananchi (CUF), kupitishwa marekebisho ya katiba na kuunda serikali ya umoja wa kitaifa visiwani humo.
Alisema jambo hilo halipaswi kubezwa wala kupuuzwa, badala yake liwe la ufuatiliaji wa hali ya juu ili kuhakikisha amani na utulivu vinadumu Zanzibar na kupatikana maendeleo kwa Wazanzibari na Watanzania kwa jumla.
“Nilichotaka kusema ndugu waandishi, sote tumeridhika na maridhiano, sote tumeridhika na uundaji wa serikali ya umoja wa kitaifa na nasema sote Wazanzibari ni washindi katika siasa hii ambayo ni ya kihistoria iliyofanyika Oktoba 31 Zanzibar,” alisema.
Hata hivyo, alisema umefika wakati kwa viongozi na wanaCCM kwa jumla Zanzibar kukaa na kufanya tathmini kuhusu Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 31, mwaka huu kutokana na chama hicho kukosa ushindi wa kishindo katika uchaguzi huo kinyume na ilivyokuwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005.
“Kama mnavyojua ndugu waandishi, ushindi haukuwa wa kishindo kama tulivyokuwa tunatarajia, na tukienda kwenye historia ya nyuma miaka mitano kumi, miaka mitano iliyopita tulikuwa katika asilimia 53, lakini Oktoba 31, mwaka huu, Zanzibar tumekuja na asilimia 50 nukta,” alisema.
0 Comments