Serikali ya Uingereza inafikiria kuyatoza faini makampuni yanayomiliki viwanja vya ndege, ikiwa safari za ndege zitasimamishwa kwa sababu hayakujiandaa vya kutosha kukabiliana na hali mbaya ya hewa.
Waziri wa uchukuzi wa Uingereza Philip Hammond, alisema hayo, alipohojiwa na gazeti la Sunday Times, baada ya theluji na barafu, kufunga uwanja mkubwa kabisa wa ndege wa London, Heathrow, ambapo safari za ndege zilisimamishwa na wasafiri walilazimika kulala sakafuni katika jumba la uwanja huo.Naye Waziri wa safari za anga, Theresa Villiers, amesema viwanja vya ndege vinahitajika kufanya kazi zake inavyotakiwa na kujiandaa ipasavyo.
Heathrow, moja ya viwanja vya ndege vikubwa duniani vyenye kupokea abiria wengi kila siku, kiliathirika zaidi wiki iliyopita kutokana na theluji nyingi kuanguka nchini Uingereza na kampuni inayoendesha uwanja huo, BAA, ilituhumiwa kushindwa kuwekeza vya kutosha katika zana za kuondoa theluji.
BAA, yenyewe inayofanya uchunguzi kubaini wapi palikwenda mrama, imesema inaafiki sheria hiyo mpya ili kuwapatia abiria huduma nzuri.
0 Comments