Magari yote yanayoingia katikati ya mji wa Zanzibar yataanza kutozwa ushuru kama utekelezaji wa mpango wa kuongeza mapato ya Baraza la Manispaa ya Zanzibar na kupunguza msongamano wa magari.
Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa ya Zanzibar, Rashid Ali Juma, alisema utekelezaji wa mpango huo unatarajiwa kuanza hivi karibuni.
Alisema utaratibu huo si mgeni katika miji mbalimbali duniani, na kutoa mfano wa Jiji la London nchini Uingereza, ambako magari yote yanayoingia katikati ya jiji hilo hutozwa ushuru wa paundi saba kuchangia maendeleo ya jiji hilo.
Aliyataja maeneo yatakayoanza kutoza magari ushuru kuwa ni Amani, Daraja Bovu, Mtoni, Uwanja wa Ndege na Kiembesamaki, ambapo magari yatakayoingia mjini yatalazimika kulipia ushuru, vinginevyo hayataruhusiwa kuingia katika Manispaa ya Mji wa Zanzibar.
Hata hivyo, hakueleza viwango vya ushuru vitakavyotumika lakini aliwataka wamiliki wa magari kutoa ushirikiano ili kufanikisha mpango huo.