Kiwango cha bei ya mafuta ya petroli kimepanda kufikia viwango ambavyo haviwahi kufikiwa katika kipindi cha miaka miwili kutokana na hofu iliyosababishwa na ghasia nchini Libya zinazotishia kuathiri mtiririko wa mafuta yanayotoka mashariki ya kati.
Bei ya mafuta ghafi ya Brent maarufu kama North Sea Brent crude yanauzwa kwa dola 117 kwa pipa moja.
Bei ya petroli kimataifa imepanda kwa asilimia 5 tangu machafuko ya Libya yaanze.
Libya ni ya 12 kati ya nchi zinazozalisha mafuta duniani, na hivyo haipo
miongoni mwa nchi zinazouza mafuta kwa wingi, ingawa mafuta ghafi ya Libya yanapendwa mno kwa sababu inaaminika kuwa kiwango chake ni cha juu na mepesi kusafisha.
Hofu iliyopo katika masoko siyo kupoteza mafuta ya Libya bali ni machafuko hayo kuenea kote katika nchi za Mashariki ya kati, hususan Saudi Arabia.
Kupanda kwa bei kwa sasa hivi kumetokana na ripoti iliyochapishwa na benki ya kuwekeza ya Goldman Sachs ikionya juu ya kupungua kwa mafuta yanayoagizwa.
Bei ya mafuta ghafi ilipanda kwa dola saba katika muda wa dakika 90 katika masoko ya hisa ya Ulaya mapema leo, ishara ya hofu iliyoyakumba masoko ya mafuta.
0 Comments