Aliyekuwa Rais wa Tunisia Zine al-Abidine Ben Ali anaumwa sana na amelazwa katika hospitali ya Saudi Arabia.
Mtu wa karibu wa familia yake ameliambia shirika la habari la AFP, Bw Ben Ali, aliyeondolewa wakati wa ghasia zilizoibuka mwezi uliopita, amepata kiharusi.

Bw Ali mwenye umri wa miaka 74 alikimbilia Saudi Arabia na familia yake baada ya kuwepo maandamano makubwa kwa wiki kadhaa juu ya ukosefu wa ajira na umaskini.
Tunisia kwa sasa ina serikali ya mpito inayoiandaa nchi kwa uchaguzi mkuu.
Jamaa huyo, ambaye jina lake halikutajwa, alisema aliyekuwa Rais yupo "kwenye hali ya kuzimia" katika hospitali moja mjini Jeddah.
Alisema, "alipata kiharusi , na hali yake ni mbaya sana."
Gazeti la Tunisia liitwalo Le Quotidien pia liliripoti siku ya Alhamis kwamba Bw Ben Ali amepata kiharusi.
Wakati huo huo, chanzo cha Saudi Arabia kilichonukuliwa na shirika la habari la Reuters limesema Bw Ben Ali alikuwa "katika hali mbaya."
Awali, msemaji wa serikali ya mpito ya Tunisia amekataa kuthibitisha au kukubali taarifa zozote kuwa Ben Ali yuko hospitali.
Ghasia za Tunisia zilimaliza miaka 23 ya utawala wake.
Japokuwa alikuwa akisifiwa kwa kudhibiti hali ya kisiasa na kuimarisha uchumi, wakosoaji wanasema alikuwa haheshimu haki za binadamu na demokrasia- madai anayoyakanusha.