MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi, Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi, imemhukumu Mayunga Samike (44) kifungo cha miaka 30 jela baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumbaka bintiye mwenye umri wa miaka 13 anayesoma darasa la tano.
Katika utetezi wake, Samike aliieleza mahakama kwamba, aliyefanya kosa hilo si yeye bali ni nguvu za mapepo zilizomwongoza.

Samike, mkazi wa kijiji cha Kakese katika kata ya Kabungu wilayani humo amehukumiwa pia kuchapwa viboko vitatu mara atakapoanza kutumikia kifungo hicho.Awali mtuhumiwa huyo, alikiri kutenda kosa hilo na kudai kuwa analijutia tendo hilo kwa sababu wakati akilitenda hakuwa na fahamu yoyote kwani alikuwa amezidiwa na nguvu ya ibilisi.

Hukumu hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki katika mahakama hiyo na Hakimu Mkazi, Desderius Magezi baada ya kuridhishwa na ushahidi ulitolewa na upande wa mashtaka.

Kabla ya kutoa hukumu, Hakimu Magezi alimtaka mshitakwa ajitetee, Samike akaiomba mahakama hiyo, impunguzie adhabu kwa kuwa mke wake ni mjamzito na tayari ana watoto wawili ambao wanahitaji malezi yake.

Alisisitiza kwamba , alitenda kosa hilo kwa bahati mbaya baada ya ibilisi kumzidi nguvu.

Hakimu Magezi alisema, ametoa adhabu kali kwa ili iwe fundisho si tu kwa Samike, bali pia kwa wazazi wengine wenye tabia kama hiyo.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, mshitakiwa huyo, alitenda kosa Februari 12, mwaka huu, saa 12:00 asubuhi maeneo ya mashambani nje kidogo na makazi yao, baada ya kumshawishi bintiye kwenda naye shambani ili amsaidie kupanda mpunga.

Baada ya kufika katika shamba lake, alimkamata kwa nguvu na hatimaye akaanza kumbaka huku mtoto akiomba msaada kwa kupiga kelele, Samike alikimbia na kutokomea kusikojulikana.

Ilidaiwa kuwa, muda mfupi baadaye , wasamaria walifika katika eneo hilo na kumkuta binti huyo, akiwa anatokwa na damu sehemu zake za siri, akilia kwa maumivu aliyoyapata na alipohojiwa alikiri kubakwa na baba yake mzazi.

Juhudi za kumtafuta zilizaa matunda ambapo alikamatwa na kufikishwa mahakamani.