SERIKALI ya Marekani imeahidi kuendelea kuisaidia Tanzania ili ifanikishe mipango yake ya kuwaletea maendeleo wananchi.
Ahadi hiyo imetolewa na Balozi wa Marekani nchini, Alfonso Lenhardt wakati alipozungumza na Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal alipomtembelea ofisini kwake Ikulu, Dar es Salaam.
Balozi Alfonso alisema kupitia mpango wa Akaunti ya Changamoto za Milenia (MCA), Serikali ya Marekani itaisaidia Tanzania kuweza kutekeleza mradi wa kuboresha miundombinu ya usafiri nchini, nishati na maji.
Alisema tayari makandarasi wapatao sita wako nchini kwa ajili ya ujenzi wa barabara za Tanga-Horohoro, Songea-Namtumbo, Peramiho-Mbinga, Laela- Sumbawanga na Tunduma-Ikana na pia kuna barabara zipatazo tano za vijijini huko Pemba zitajengwa.
Balozi Alfonso alisema Serikali ya Marekani imesaidia katika sekta ya elimu na kilimo hasa cha mpunga na mahindi katika mikoa ya Morogoro na Manyara na mbogamboga kwa Morogoro na Zanzibar.
“Mradi huu umeandaliwa kukifanya kilimo kiweze kuchangia katika kuinua uchumi wa nchi pia kuwawezesha wananchi kupata maendeleo,” alisema na kuongeza “Tanzania ina maji na ardhi
ya kutosha, ina watu wenye nguvu za kufanya kazi.
Mradi huu una lengo la kukibadilisha kilimo ili kiweze kuwanufaisha wananchi wenyewe.” Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Rais aliishukuru Marekani kwa misaada mbalimbali na kuelezea kufurahishwa kwake na mradi wa kilimo; aliosema utasaidia utekelezaji wa kaulimbiu ya Kilimo Kwanza.
Katika hatua nyingine, Dk. Bilal alikutana na Balozi wa Afrika Kusini nchini, Thanduyise Chiliza ambapo walizungumzia umuhimu wa Afrika kufanya kazi pamoja kwa lengo la kuliletea maendeleo Bara la Afrika.
Pia alikutana na Balozi wa Cuba nchini, Ernesto Gomez kusisitiza umuhimu na kukuza
ushirikiano.
0 Comments