WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema kamwe Serikali haiwezi kutoa tamko dhidi ya polisi wa Arusha kwa tukio la vurugu za kisiasa lililotokea hivi karibuni, kwa kuwa Jeshi hilo halikuanzisha hizo vurugu.

Pia ameishauri Chadema kutumia busara na kujijenga kwa manufaa ya baadaye badala ya kuendekeza tabia za kususa na kuhamasisha vurugu, jambo ambalo ni hatari kwa Taifa. Alisema hayo Alhamisi bungeni mjini hapa wakati wa kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu, wakati alikuwa akijibu swali la Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe (Chadema) aliyetaka kujua hatua zinazochukuliwa dhidi ya polisi wa Arusha kwa vifo vya watu watatu kwenye vurugu hizo.

Pinda alisema si busara kwa watu kukimbilia kuilaumu Serikali kutokana na tukio la Arusha na badala yake wangejiuliza kwanza, nani aliyesababisha mauaji ya watu hao.

“Nasikitika katika hili tumepoteza Watanzania bila sababu, ila nataka kuwaambia kuwa Serikali iko makini, na si vyema kuilaumu kuhusu suala hili, angalieni kwanza chanzo,” alisema Pinda.

Alisema Chadema waliomba kibali cha maandamano na kukubaliwa na Polisi lakini kwa masharti ya kutumia njia moja mjini Arusha, lakini chama hicho kilikataa na kutaka kutumia njia zote, jambo ambalo kutokana na udogo wa mji huo, Polisi ilihofia vurugu na kukataa kutoa kibali hicho.

“Sisi tulikataa kukubali ifanyike mnavyotaka ninyi, ndiyo maana tuliruhusu tu mkutano wa kawaida, ambao mliukataa na kulazimisha kufanya maandamano hivyo kilichotokea katika harakati za kuzuia maandamano baadhi yenu walikamatwa na Polisi,” alisema Waziri Mkuu.

Alisema Serikali ilishukuru kuona kuwa chama hicho mwishowe kiliamua kufanya mkutano wa hadhara ambao hata hivyo ulitumika kwa viongozi wa chama hicho kukashifu na kutoa maneno ya uchokozi na kuhamasisha wafuasi wake zaidi ya 2,000 kuvamia kituo cha Polisi ili kuwatoa wenzao waliokamatwa.

Alisema kituo kilichovamiwa ni kikubwa na chenye silaha kama vile bunduki na mabomu, hivyo baada ya kuona kundi hilo likisogea karibu, askari walijaribu kujihami kwa kuanza na mabomu ya machozi, lakini baadaye walishindwa kuwamudu wananchi hao ambao walisogelea kituo hicho kwa takribani meta 50.

Waziri Pinda alisema kutokana na wingi wa watu, kuliibuka vurugu na purukushani ambazo kwa bahati mbaya zilisababisha vifo vya watu hao watatu. Waliouawa ni Watanzania wawili na Mkenya mmoja.

“Ninachotaka kusisitiza hapa ni kwamba iwapo Chadema wangekubaliana na matakwa ya Serikali ya kutumia ruti moja kuandamana au kufanya mkutano wa hadhara pekee, haya yote yasingetokea,” alisisitiza.

Aliwataka wananchi wafahamu kuwa haiwezekani askari wale wakaamua kufyatua risasi na mabomu ovyo bila sababu ya msingi. “Rai yangu ni kushirikiana tujenge Taifa lenye amani na upendo.”

Alikishauri chama hicho kujijenga kwa kuwa makini zaidi, kwani matukio yake ya hivi karibuni akitoa mfano wa Arusha, kususia hotuba ya Rais Jakaya Kikwete wakati akifungua Bunge la 10 mwaka jana na kususia majadiliano juu ya tafsiri ya kanuni ya kambi ya upinzani bungeni, yanaweza kukiharibia.

“Mimi nawashauri tu tabia hii ya kususa na kutoka nje ya Bunge wakati vikao vya chombo hiki vikiendelea, haiwezi kukijenga chama hiki, kuweni makini ili chama chenu kiwe imara na hata ikitokea tunatakiwa kuachiwa madaraka kama CCM, tunajua kabisa tunaachia chama kinachoaminika,” alisema.

Akijibu swali la nyongeza la Mbowe aliyetaka kujua kama Serikali itaunda tume kuchunguza chanzo halisi cha vurugu za Arusha, Pinda alisema:

“Mheshimiwa Mbowe kama dhamira yako ni nzuri, usingesubiri kufikisha wazo lako hili hapa bungeni, sawa umesema uchunguzi ufanyike, lakini ni lazima tujiridhishe kwanza kama zipo sababu za kufanya hivyo.”

Alhamisi Mbowe alikaririwa akisema Chadema itaendelea kususia Bunge na kutoka nje iwapo wataona hawatendewi haki katika uamuzi mbalimbali na lengo lao ni kufikisha ujumbe wa kutoridhishwa.

Wakati huo huo, baadhi ya wabunge wamesema umefika wakati wa kuacha majoho ya vyama vya upinzani na kuungana kuyatafutia ufumbuzi matatizo yanayowakabili Watanzania kwa sasa hususani katika elimu.

Na kuhusu tatizo la wanafunzi wa kidato cha nne kufeli kwa kiwango kikubwa, wameiomba Serikali iangalie namna ya kuwasaidia ili kunusuru maisha yao.

Akichangia mjadala wa hotuba ya Rais Jakaya Kikwete, Alhamisi jioni, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, alisema kwa sasa Taifa lina matatizo mengi yakiwamo ya elimu na uchumi, hali inayohitaji ushirikiano wa hali ya juu.

“Jamani hata sisi vijana tuliomo humu ndani tuungane bila kujali vyama vyetu, tuangalie namna ya kuikabili hali hii, haya matatizo yote tunayoyaona yanatokana na matabaka yaliyojengeka ya walio nacho na wasio nacho,” alisema.

Naye Mbunge wa Tarime, Nyambari Nyangwine (CCM), aliitaka Serikali kuboresha huduma za usafiri zinazoweza kuitangaza Tanzania duniani na kupunguza urasimu bandarini.

Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohammed (CUF), aliiomba Serikali ipeleke kesi zote za rushwa bungeni ili kuondoa utata baina ya Mwendesha Mashitaka wa Serikali na Mwanasheria Mkuu kuhusu kuchelewa kufikisha kesi hizo mahakamani.