Mwanamke mmoja aliyetambulika kwa jina la Amina Ramadhani mwenye umri kati ya 25 na 30 amekutwa amefariki dunia katika nyumba ya kulala wageni ya Mkombozi, Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alisema tukio hilo lilitokea juzi, ambapo maiti ya mwanamke huyo ilikutwa ikiwa kitandani ikiwa imefunikwa khanga na mwili kutokuwa na jeraha lolote.
Alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa Februari 23, mwaka huu majira ya saa saa 7:00 mchana, marehemu alifika katika nyumba hiyo akiwa ameongozana na
mwanaume ambaye hakufahamika jina na kupanga chumba namba sita.
Alisema baada ya kukaa kwa muda mrefu katika chumba hicho, mwanamume huyo alimuaga muhudumu kwamba anakwenda kutafuta chakula cha mchana huku akiacha mlango wa chumba hicho wazi.
Kenyela alisema, mmoja wa wahudumu katika nyumba hiyo, alikuta mlango huo ukiwa wazi na alipojaribu kumwamsha mteja wake afunge mlango, lakini hakuweza kuamka.
Pia, ilibaini kuwa marehemu alikuwa na vitambulisho viwili ambapo kimoja kilikuwa cha Ubungo High School, kikiwa na jina la Amina A. Ramadhani kilichokuwa kikionyesha alianza kidato cha kwanza mwaka 1996 hadi 1999 alipomaliza kidato cha nne.
Kitambulisho cha pili kilionyesha jina la Ramadhani Abdul mpishi, kilichotolewa na Dar es Salaam College of Technology, kwa Sanduku la barua 2958 na namba ya simu 150824.
Maiti ya mwanamke huyo imehifadhiwa katika Hospitali ya Mwananyamala kwa uchunguzi.