WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, amewashangaa viongozi waandamizi wastaafu serikalini na CCM kuacha kuzungumzia malalamiko yao katika vikao halali kabla ya kukimbilia kwenye vyombo vya habari.
“Vyama vina mifumo yao ya kuendesha shughuli zao … vina maeneo ya kusemea mambo yao na huko ndiko kusaidia chama na kuweka mikakati ya kukiendeleza,” alisema Waziri Mkuu alipozungumza na wahariri wa vyombo vya habari mjini Dar es Salaam jana.
Alikuwa akijibu swali kuhusu viongozi wa CCM wakiwamo wastaafu, kulumbana na umoja wa vijana wa chama hicho hadharani badala ya kutumia vikao halali vilivyopo.
Alisema kutoa madukuduku kwa kutumia magazeti kabla hata ya kukataliwa katika vikao halali vilivyopo, si dhamira nzuri.
“Kama malalamiko yako uliyatolea katika vikao halali na ukakataliwa kusikilizwa na hivyo ukaamua kutoka na kuyasema nje, hilo halina tatizo. “Na hasa viongozi wastaafu. Hawa wana fursa ya ziada, wana uhuru hata wa kumwona Rais na kusema naye, wakitumia uzoefu walionao kumsaidia hata yeye,” alisema Pinda.
Aliasa kuwa si picha nzuri kuona kana kwamba viongozi hao wanakataliwa kusikilizwa katika vikao na hivyo kuamua kuyasema hadharani. ”Msiwe waoga kusema ndani ya vikao halali kwani huko ndiko hasa pa kujenga na si kusemea kwingine … huko ndiko kukisaidia chama na kupanga mikakati zaidi ya kukiimarisha,” alishauri Pinda.
Hivi karibuni, yamekuwapo malumbano baina ya viongozi wastaafu wa CCM na Serikali yake pamoja na viongozi wa Jumuiya ya Vijana ya CCM (UVCCM), baada ya viongozi hao kuzungumzia hoja za Chadema na kuitaka CCM izijibu.
UVCCM ilitupa lawama kwa viongozi hao akiwamo Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye, Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa na Spika wa zamani wa Bunge, Samuel Sitta kuhusu kuzisema CCM na UVCCM hadharani badala ya kufuata vikao halali.
Wiki iliyopita, Sumaye akizungumza na vyombo vya habari kujibu tuhuma za UVCCM dhidi yake, alisema wanapotoka na kuwataka wajirekebishe, huku akiwatuhumu kwa kutoa kauli zinazoashiria kuwa wana mgombea wao wa urais wa mwaka 2015 wanamwandaa.
Kuhusu hali ya umeme, Waziri Mkuu alisema kuna unafuu kidogo kutokana na mvua zinazonyesha, ambazo zimeongeza kina cha maji katika mabwawa ya Kidatu na Kihansi, lakini Mtera hali bado si nzuri kutokana na Mto Ruaha kutokuwa na maji ya kutosha.
Akizungumzia Serikali kutotoa tamko lolote kuhusu Libya kushambuliwa na majeshi ya kigeni, Pinda alisema anatambua uhusiano na urafiki uliopo baina ya nchi hiyo na Tanzania, lakini akasema kwa sasa Serikali haiwezi kusema lolote ila itaheshimu uamuzi na msimamo wa pamoja wa Umoja wa Afrika (AU).
Kuhusu hali ya chakula, alisema bado kipo cha kutosha na kwamba kwenye maeneo yenye upungufu uliosababishwa na ukosefu wa mvua, Serikali imeshasambaza tani 13,000 na zimechukuliwa na halmashauri husika, na kuzitaka zenye matatizo ziseme ili zisaidiwe haraka.
Juu ya suala la matrekta madogo, Waziri Mkuu alisema si kwamba yana matatizo ila inategemea na aina na pia maeneo yanakopelekwa kufanya kazi.
“Matrekta haya ndio mbadala wa jembe la mkono, huwezi kumrusha mkulima mdogo kutoka jembe la mkono hadi trekta kubwa, ni aghali.
Lakini matrekta madogo yanastahili kilimo cha tambarare na si milimani … tuhakikishe tu
yamethibitishwa na vyombo husika,” alisema.
Akizungumzia uhaba wa sukari, alisema ni jambo lililopangwa kwa makusudi na wafanyabiashara wa chini, kwa sababu sukari ipo ya kutosha na kuwataka maofisa biashara nchini kuingilia kati ili kudhibiti udanganyifu unaofanywa kwa kisingizio cha hali ngumu ya maisha.
Kuhusu foleni Dar es Salaam, Waziri Mkuu aliahidi kuyafanyia kazi mawazo aliyopewa na wahariri hao yakiwamo ya kuyapangia muda, malori ya mizigo yapitayo barabara ya Nelson Mandela, wa kuingia na kutoka bandarini asubuhi na jioni.(Habari kamili toka Habari leo).
0 Comments