Walimu wa shule za msingi na sekondari nchini, wametakiwa kufuata kanuni na sheria ya adhabu ya viboko kwa mwanafunzi pindi anapofanya kosa kama serikali ilivyopanga.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba, wakati wa kikao cha kujadili namna ya kudhibiti tatizo la watoto waishio mitaani jana, jijini Dar es Salaam.
Alisema walimu wengi wamekuwa wakikiuka sheria inayowataka kuwaadhibu wanafunzi viboko vinne tu, lakini wanazidisha na kusababishia matukio ya kikatili wanayoyafanya juu ya watoto hao.

“Sheria inakataza mwalimu kumchapa mwanafunzi, lakini tukaona bila viboko wengine hawaendi hivyo ikawekwa adhabu ya viboko kwa mtoto mwisho ni vinne na tena mpaka huyo mwalimu apate kibali kutoka kwa mkuu wa shule na si kinyume na hapo, lakini tunaona wanavyowaadhibu watoto wetu mpaka kuwajeruhi hivyo kama mzazi kaona mwanae kapatwa na tatizo hilo basi haraka akatoe taarifa polisi,” alisema Simba.
Pia alielezea suala la wazazi kuwaadhibu watoto wao adhabu kubwa kuliko umri wao ni jambo linaloweza kuwa moja ya vyanzo vya ongezeko kubwa la watoto waishio mitaani katika mazingira hatarishi.
“Tunasikia matukio mengi sana ya kikatili kwa kipindi hiki yanayotokea katika nchi hii juu ya watoto kutendewa na walimu wao na hata wazazi, kweli haya ni makosa na ni kinyume na haki za watoto ambazo kila kukicha wanazililia katika jamii zao ikiwemo ya kupata upendo kutoka katika familia zao,” alisema Simba.
Afafanua kuwa, katika utafiti uliofanyika Agosti, 2009 na kufadhiliwa na Shirika lisilo la kiserikali la Uingereza la Consortium for Street Children unaoonyesha kuongezeka kwa kasi tatizo hilo.
Utafiti huo ulifanyika katika miji ya Dar es Salaam, Morogoro, Iringa, Mbeya, Dodoma, Singida na Moshi ambapo jumla ya watoto 2,295 walifanyiwa utafiti wakiwemo wasichana 538 na wavulana 1,757.
CHANZO: NIPASHE