Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), imeuagiza Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF), kuipa notisi Kampuni ya Quality Group Limited inayomilikiwa na Yusufu Manji, kuhama mara moja katika jengo la Quality Plaza linalomilikiwa na Mfuko huo.
Agizo hilo la POAC linatokana na uongozi wa Quality Group Limited, ambaye ni mpangaji katika jengo hilo, kushindwa kulipa Sh. bilioni 5 zikiwa ni limbikizo la kodi ya upangaji katika kipindi cha miaka minne, kuanzia mwaka 2006.

Mwenyekiti wa POAC, Zitto Kabwe, alithibitisha kamati yake kuiagiza PSPF kuipelekea Quality Group Limited notisi hiyo jana.
Kwa mujibu wa Zitto, agizo hilo lilitolewa baada ya kamati yake kukagua hesabu za PSPF walipokutana katika Ofisi Ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam jana.
Zitto, ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), alisema kikao hicho kati ya POAC na PSPF kilijikita katika kujadili taasisi zote zinazodaiwa na Mfuko huo.
Alisema baada ya mjadala huo, ilibainika kuwa miongoni mwa wadaiwa wa PSPF, ni pamoja na Quality Group Limited.
Kabla ya PSPF kumiliki jengo hilo lililoko Barabara ya Nyerere (zamani Pugu Road), lilikuwa likimilikiwa na Manji kupitia kampuni yake ya Quality Group Limited.
Baadaye, Manji aliiuzia PSPF jengo hilo kwa Sh. bilioni 36 na kisha baadaye akawa mpangaji katika jengo hilo.
“Anadaiwa Sh. bilioni 5 za kodi ya upangaji kwa miaka minne, kuanzia mwaka 2006. PSPF wanasema wanapomdai anakataa kulipa,” alisema Zitto.
Alisema katika kikao hicho, uongozi wa PSPF uliieleza POAC kuwa katika kilele cha kukataa kulipa deni hilo, Quality Group Limited ilifungua kesi mahakamani kuiomba mahakama iuzuie Mfuko huo kuihamisha katika jengo hilo.
Zitto alisema kwa mujibu wa uongozi wa PSPF, mahakama ilikubaliana na ombi la Quality Group Limited, ambayo ilitoa amri ya kuuzuia Mfuko huo kuihamisha Quality Group Limited katika jengo hilo katika kipindi cha miezi sita.
Kwa mujibu wa Zitto, licha ya muda wa zuio hilo la mahakama kuisha tangu mwaka juzi, Quality Group Limited waliendelea kukaidi kulipa deni hilo la PSPF hadi sasa.
“Kwa hiyo, jana (juzi) baada ya kupata maelezo yao, kamati iliwaagiza leo (jana) PSPF waipelekee Quality Group Limited notisi ya kuwahamisha, watoke katika hilo jengo na kisha wailetee kamati nakala ya notisi hiyo,” alisema Zitto.
Zitto alipoulizwa na NIPASHE jana, alithibitisha kamati kupata nakala ya notisi ya PSPF iliyopelekwa kwa Quality Group Limited kupitia kwa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Image Properties and Estate, ambayo ni wakala wa kampuni hiyo (Quality Group Limited).
CHANZO: NIPASHE