Rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan, ambaye amechaguliwa tena kama rais wa nchi hiyo, ametoa wito kwa raia kuwa watulivu na kumaliza kile alichokitaja kuwa ghasia na mauaji yasiyohitajika, Kaskazini mwa nchi hiyo.
Rais Jonathan aliyasema hayo, baada ya kutangazwa rasmi kuwa mshindi wa uchaguzi huo wa urais.
Muda mfupi baada ya rais Jonathan, kutangazwa rasmi kama mshindi, wafuasi wa mpinzani wake mkuu Muhammadu Buhari, waliteketeza nyumba, makanisa na magari katika eneo la Kaskazini mwa Nigeria.

Rais Jonathan amesema serikali yake itachukua hatua za dharura ili kulinda maisha ya raia na mali yao.
Wafuasi wa Generali Buhari, wanaripotiwa kusababisha ghasia hizo kulalamikia kile wanachodai kuwa ni wizi wa kura.
Shirika la msalaba mwekundi nchini Nigeria, limethibitisha kuwa watu kadhaa wameuawa.
Makanisa na nyumba kadhaa ikiwemo ile ya makamu wa rais wa nchi hiyo Namadi Sambo katika jimbo la Kaduna zimeteketezwa

Ripoti zaidi zinasema wafuasi hao wa Buhari walivamia gereza moja na kuwaachilia huru wafungwa wote.
Hata hivyo, akizungumza na BBC msemaji wa Generali Buhari, amekanusha madai ya kuuawa kwa watu kadhaa Kaskazini mwa nchi hiyo.
Ameongeza kuwa mwenyekiti wa chama chao tayari ametoa wito kwa raia kuwa watulivu.