Wakati sikukuu ya Pasaka inakaribia, Mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Mwasapila, ameelemewa tena na umati wa watu na kusababisha magari kufikia umbali wa kilomita 25 kutoka nyumbani kwake katika kijiji cha Samunge, Loliondo wilayani Ngorongoro wakisubiri kupata tiba ya kikombe.
Mchungaji Mwasapila alishatangaza siku kadhaa zilizopita kwamba atasimamisha huduma za kutoa tiba yake ya magonjwa sugu kwa ajili ya sikukuu ya Pasaka ambayo ni kumbukumbu ya kufufuka kwa Yesu Kristo.
Siku hiyo itaadhimishwa Jumapili ijayo.
Huduma za tiba ya Mchungaji Mwasapila zitasitishwa kuanzia Ijumaa Kuu hadi Jumatatu ijayo.
Kuongezeka kwa watu wanaokwenda kupata tiba hiyo kumeelezwa kuwa kumetokana na baadhi ya watu kutaka kupata kikombe cha Babu kabla ya kusitishwa kwa huduma hiyo.
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Isidore Shirima, alisema jana kuwa chanzo cha umati huo kufurika Samunge ni kutokana na watu wa Kanda ya Ziwa hasa kituo cha Bunda, mkoani Mara kukiuka taratibu kwa kupitisha wagonjwa wengi kuliko uwezo wa huduma inayotolewa.
Shirima alisema kuwa Alhamisi ya wiki iliyopita, magari mengi yaliruhusiwa kupita na kusababisha wagonjwa wengi kurundikana nyumbani kwa Babu.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini hapa Shirima, alisema kuwa kutokana na huduma hiyo kusitishwa siku hizo za Pasaka, vituo vyote vya magari ya kupeleka wagonjwa navyo vitasitisha kuruhusu magari kuanzia leo ili kumwezesha mchungaji huyo kumaliza kutoa tiba kwa umati uliopo nyumbani kwake kwa sasa.
Alisema serikali inasikitishwa na Babu kuzidiwa na idadi ya watu kwa sababu ilikuwa na lengo zuri la kuweka vituo vitatu vya Bunda (Mkoa wa Mara), Arusha (Mkoa wa Arusha) na Babati (Mkoa wa Manyara) ili kuwawezesha watu kutolala Samunge na kwamba lengo hilo siku za mwanzo lilifanikiwa ambapo watu walikuwa wakienda Samunge na kurudi siku inayofuata.
“Lakini sasa watu wanavyoshinikizwa kwa mfano wenye magari na wagonjwa. Hali hiyo inasababisha watu kuanza kufurika kijijini Samunge na kusababisha tena kijiji kuelemewa,” alisema Shirima.
Alisisitiza kwamba magari madogo na malori hayatakiwi kupeleka wagonjwa kwa Babu kwa sababu barabara bado ni mbaya na yanachangia vifo kwa wagonjwa mahututi.
“Jamani, tunaomba watu wasipeleke wagonjwa mahututi kwa Babu, kwani yeye anatoa tiba na siyo hospitali ya rufaa. Ila inasikitisha kuona watu wanapeleka wagonjwa mahututi,” alisema Shirima.
Alisema magari yanayoruhusiwa kwenda kwa Babu ni lazima yapite kwenye vituo vilivyopangwa ili kukaguliwa na lazima yafuate utaratibu wa kutembea kilomita 40 hadi 50 kwa saa moja na siyo zaidi ya hapo lengo likiwa ni kupunguza ajali zisizo za lazima.
Shirima pia aliomba wenye magari yatakapopita katika vituo lazima wahakikishe wanaandika majina ya wagonjwa waliowabeba kuwapeleka Samunge.
Alisema majina hayo yanapaswa kuachwa katika vituo hivyo kwa ajili ya kufuatilia taarifa ikiwa litatokea tatizo hasa likitokea tukio la kutelekezwa wagonjwa au maiti.
Shirima aliongeza kuwa utaratibu uliowekwa awali ulikuwa mzuri na serikali iliwapendelea watu wa Kanda ya Ziwa kwa kupeleka idadi kubwa ya watu 1,000 badala ya 500.
Hata hivyo, aliwalaumu kwamba licha ya kupewa upendeleo, lakini wanafanya vitendo vya vurugu kwa ajili ya kushinikiza kuruhusiwa watu zaidi kupita kwenda kwa Babu.
HALI YAMSIKITISHA DC
Naye Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Elias Wawa Lali, alisema kuwa anasikitishwa na hali ilivyo sasa baada ya kuzuka kwa msururu ghafla.
Alisema foleni imerejea na kwamba imerudi kama awali kabla ya kuwekwa utaratibu, na kwamba watoa huduma wameelemewa.
“Bei za vyakula pia iko juu na watu wanalalamika, lakini ili kushusha bei za vyakula watu waheshimu utaratibu uliowekwa na serikali kwa sababu huku hakuna huduma nyingi za jamii, ndio sababu serikali iliweka utaratibu,” alisema Wawa Lali.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa hali hiyo inaweza kusababisha matatizo zaidi kama awali kama wagonjwa kuchelewa kumfikia Babu, jambo ambalo siyo la busara.
“Tunaomba watu wangetumia busara na waheshimu utaratibu kwa faida yao pia na siyo kuikomoa serikali,” alisisitiza.
Mkuu huyo wa wilaya aliongeza kuwa baada ya kuona foleni ya magari imekuwa kubwa, aliamua kuwasiliana na watu wa Bunda nao wakadai wamechoshwa na lawama za wananchi, hivyo wameamua kuachia watu waende watakavyo kwa maelezo kuwa wao hawasimamii tena utaratibu wa kutoa vibali kwa magari.
“Sasa sisi huku tunateseka na umati uliopo, tunaomba watu waiheshimu serikali jamani, siyo kukiuka,” alisema Wawa Lali.
Watu wanaokwenda kwa Babu kutokea kituo cha Bunda kinachohudumia Kanda ya Ziwa mara kadhaa wamefanya vurugu kushinikiza kuruhusiwa kupita.
Katika tukio la kwanza, walifunga barabara kwa mawe na kulala katikati ya barabara hiyo na kutulizwa baadaye na Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Francis Isaack.
Katika tukio la pili, walifanya maandamano na kumpelekea Mkuu wa Wilaya maiti ya mmoja wa wagonjwa aliyefia katika kituo hicho akitokea wilayani Kahama.
Vurugu hizo katika kituo cha Bunda mara kadhaa zimemlazimisha DC Isaack kuingilia kati kutoa maelekezo kuhusiana na utaratibu wa kuruhusu magari kwenda kwa Babu.
CHANZO: NIPASHE
0 Comments