Mamia ya wananchi wanaokwenda kwenye tiba ya Mchungaji Ambilikile Masapila katika Kijiji cha Samunge-Loliondo, wilayani Ngorongoro, kupitia kituo cha Bunda, mkoani Mara, juzi walitawanywa na polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) baada ya kuziba barabara kuu ya Mwanza-Musoma na kuzuia magari kupita kwa zaidi ya saa nne.
Wananchi hao waliandamana na kwenda katika makutano ya barabara hiyo na ile ya Mugumu-Ukerewe na kuziba kwa mawe, kukaa na wengine kulala chini wakishinikiza serikali kuwapa vibali vya kwenda kwa Babu.
Walifikia uamuzi huo baada ya mwili wa mgonjwa mmoja mwanaume, mkazi wa wilayani Kahama, aliyefariki dunia akiwa kituoni hapo, ulipopelekwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Bunda Francis Issack, aliyekuwa akitoa utaratibu wa kuruhusu magari yaliyopatiwa vibali.
Baada ya Isaack kutoka katika eneo hilo saa 10:15 jioni, wananchi waliandamana na kwenda kuziba barabara hiyo na kuzuia magari kupita, hali iliyosababisha msongamano mkubwa wa magari.
Pamoja na mvua kunyesha, wananchi hao waliendelea kushikilia msimamo wao wa kuzuia eneo hilo.
Hata hivyo, ilipofika saa 2:00 usiku, kikosi cha askari wa FFU kutoka Musoma, walifika na kuwatawanya.
Wakati huo huo, vibali vya magari ya kupeleka wagonjwa kwa Mchungaji Masapila, kwa ajili ya kupata tiba ya magonjwa sugu, vimezuiwa kwa muda ili kupunguza idadi ya watu waliokwama kijijini hapo tangu juzi.
Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Elias Wawa Lali, alisema vibali hivyo vimezuiwa kwa muda hadi watu watakapopungua.