Makundi mawili yanayozozana ya Fatah na Hamas yamesema yamekubaliana kuunda serikali ya mpito ya muungano huko Palestina.
Habari hii muhimu ilitangazwa nchini Misri, nchi ambayo imekuwa inajaribu kupatanisha makundi haya.
Mapigano ya makundi hayo mawili yalianza miaka minne iliopita yakiacha kundi la Fatah likidhibiti eneo la West Bank na Hamas eneo la Gaza.
Lakini hatua hii ya kuafikiana imepingwa na Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ambaye anasema kundi la Fatah linaloongozwa na Rais Mahmoud Abbas haliwezi kufanya amani na Israel na Hamas.
Bw Netanyahu anasema lengo la Hamas ni kuangamiza Israel na kuwa hatua hii inaonyesha ulegevu wa utawala wa Rais Abbas.
Mgawanyiko kati ya Hamas na Fatah ni mkubwa na wakati mwengine kumekuwepo na maafa.
Vyombo vya usalama kutoka pande zote vimekuwa vikizozana na kuna hofu ikiwa vitaweza kuweka tofauti zao kando na kutii amri kwa utawala mmoja.
Kulingana na makubaliano hayo, Hamas watasimamia usalama wa Gaza na Fatah watadhibiti eneo la West Bank.
Ni wazi kuwa Rais Abbas amekerwa na kukwama kwa mazungumzo ya amani kati yao na Israel ndio maana ameamua kukubaliana na Hamas.
Serikali ya Marekani na Umoja wa nchi za Uropa wanalitambua kundi la Hamas kama magaidi, na haijulikani ikiwa wataendelea kufadhili utawala wa Rais Abbas baada ya muafaka huu.
0 Comments