Mkurugenzi wa Hoteli ya South Beach Salim Nathoo akijikinga na kitambaa asipigwe akiwa na mshtakiwa mwenzake John Mwangiombo wakipelekwa katika chumba cha Mahakama ya Wilaya ya Temeke jijini 
Mkurugenzi wa Hoteli ya Kitalii ya South Beach ya jijini Dar es Salaam, Salim Nathoo maarufu kwa jina la Chipata (53), amepandishwa kizimbani akikabiliwa na kesi ya mauaji ya kumchoma moto kijana aliyeingia kwenye hoteli yake bila kibali.
Nathoo, mkazi wa Mikocheni A alifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Temeke, Khasim Mkwawa, jana akiwa pamoja na mshitakiwa mwenzake John Mwangiombo (32), kujibu tuhuma za mauaji.
Akisoma hati ya Mashtaka, Mwendesha Mashtaka Inspekta wa Polisi Dastan Kombe aliiambia Mahakama hiyo kuwa Aprili 10 mwaka huu majira ya saa 6.30 usiku eneo la Mjimwema Kigamboni, washitakiwa walishirikiana kumpiga na kumchoma moto Lila Hussen (34) na kumsababishia kifo.
Hata hivyo, Hakimu Mkwawa aliwataka washtakiwa wote kutojibu shtaka hilo kwa kuwa Mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza na kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 2, mwaka huu kwa kutajwa tena.

Hata hivyo, ndugu wa marehemu Lila hawakufika mahakamani kwa kile kilichoelezwa kuwa walikuwa wanashughulikia utaratibu wa mazishi wa ndugu yao.
Inadaiwa alichomwa moto na washtakiwa baada ya kuingia hotelini hapo kwa ajili ya kuwatafuta wageni wake, ambapo washtakiwa hao walimwagia mafuta na kumvisha tairi na baadaye kumuwasha kwa kibiriti.
Hata hivyo, marehemu kabla ya kifo chake alilazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Akithibitisha kifo hicho, Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Devid Misime, alisema Lila alifariki usiku wa kuamkia juzi hospitalini hapo baada ya juhudi za madaktari kuokoa maisha yake kushindikana.
CHANZO: NIPASHE