SPIKA wa Bunge, Anne Makinda amesema hatishiki na yale yanayotokea ndani ya Bunge kwa baadhi ya wabunge kusababisha mabishano na malumbano, akidai Bunge la Tanzania analoliongoza ni miongoni mwa mabunge tulivu duniani.

Aidha, aliongeza kusema kwa kuwa anafahamu vyema kanuni za Bunge lake, lakini analazimika kutumia busara kuliendesha huku akisisitiza kuwa, kama akiamua kutumia sheria, baadhi ya wabunge wataondolewa kwa kubebwa na polisi.


Makinda aliyasema hayo jana wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro wakati anazungumza na madiwani wa Halmashauri ya Wilaya hiyo alipowasili wilayani humo kwa ajili ya kuendesha harambee ya uchangiaji wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mtakatifu Theresa.


Alisema yupo wilayani humo kwa mwaliko wa shule hiyo ambayo inamilikiwa na Kanisa Katoliki, lakini pia lengo la kuchangia upatikanaji wa elimu kwa watoto wa kike lilimgusa zaidi na kukubali mwaliko huo.


Spika Makinda alisema, Bunge la Tanzania ni tulivu mno ikilinganishwa na mabunge mengine na kuongeza kuwa malumbano yanayotokea sasa yanasababishwa na baadhi ya wabunge kutoelewa kanuni ipasavyo.


“Waheshimiwa madiwani mimi sina neno na hayo yanayotokea ndani ya Bunge, lakini hata hivyo huwa natumia busara kuliendesha lile Bunge…wakati mwingine nikiamua kutumia sheria, baadhi ya wabunge wataondolewa pale kwa kubebwa na polisi,” alisema.


Aidha, Makinda alisema yeye amekuwa ndani ya Bunge kwa takribani miaka 36 hivyo anafahamu vyema kanuni, lakini baadhi ya wabunge hufanya makusudi kusababisha malumbano ili yeye achukue sheria ambazo wakati mwingine zitasababisha vurugu.


“Lipo jambo wanataka nilifanye kisha zitokee vurugu za kudumu…mimi najua nini wanataka, nitaendelea kuwaelimisha kanuni na taratibu za vikao vya Bunge,” alisema.


Hata hivyo Spika Makinda alielezea jinsi anavyokerwa na baadhi ya wasomi ambao huwapotosha wananchi kuhusu Muswada wa kuundwa kwa tume itakayoratibu mchakato wa wananchi kutoa maoni kuhusu Katiba mpya.


Alisema wasomi hao ambao wamesoma robo ya elimu inayohitajika, wamelenga kufanya upotoshwaji ili wananchi waamini kwamba Serikali imeandaa Muswada wa Katiba mpya jambo ambalo halikuwa na ukweli wa aina yoyote.


Alisema Muswada ambao ulisababisha baadhi ya wasomi kuzomea bila kujua nini kimeandikwa, ulikusudia kupata maoni ya wananchi juu upatikanaji wa tume hiyo kulingana na mapendekezo ya Rais Jakaya Kikwete.


“Baadhi ya wasomi wetu wamepata elimu robo robo, wameshindwa kuelewa Muswada unataka nini….hawa ni watu wa kuelimisha wananchi kweli, wengine wanazomea kiholela tu bila kuusoma vyema,” alisema.


Alisema Muswada huo uliwasilishwa katika Mkutano wa Tatu wa Bunge, lakini kabla haujasomwa mara ya pili wananchi walipata fursa ya kutoa maoni katika vituo vya Dodoma, Dar es Salaam na Zanzibar, lakini kuliibuka vurugu zilizosababisha kurejeshwa serikalini.


Hata hivyo alisema Kamati za Bunge zilizokuwa zikiratibu maoni hayo zilipata maoni mengi ambayo yatafanyiwa kazi ili kuhakikisha Taifa linapata utaratibu ambao utasaidia upatikanaji wa Katiba mpya.