WATU 13 wamekufa papo hapo na wengine 12 wamejeruhiwa baada ya basi walilokuwa wakisafiria mali ya Kampuni ya Sumry, kupasuka tairi la mbele katika eneo la Igawa wilayani Mbarali mkoani Mbeya.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Advocate Nyombi alisema ajali hiyo iliyotokea saa nne usiku wa kuamkia jana. Basi hilo aina ya Nissan lilikuwa likitoka Arusha kwenda Mbeya.
Aliwataja watu waliokufa kuwa ni pamoja na dereva wa basi hilo, Makame Juma (54), Mwalimu wa Shule ya Msingi Ubaruku wilayani Mbarali, Florence Kitaule (41), Bupe Mwaijumba, Magret Komba na Kandi Komba.
Wengine ni Gasper Lupoli na Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Kampasi ya Mbeya, Thomas Chalo (28). Miili ya watu wengine saba bado haijatambuliwa.
Aliwataja watu waliojeruhiwa katika ajali hiyo kuwa ni Twarub Fakir, Lupi Mwaipalo, Martin Costantine (25), Thader Legate (43), Andrew Adolf (32), Anael Kibete, Ezekiel Adolf, Riziki Chuwa (25) na Erasto Kiwaga.
Wengine ni Hassan Mohamed, Bakari Kayumba na Halima Abdalla na majeruhi wamelazwa katika hospitali ya Wilaya ya Mbarali kwa matibabu.
Alisema kati ya watu 13 waliokufa, wanaume ni wanane na wanawake ni watano na amewataka wananchi kujitokeza kuitambua miili ya watu hao saba hiyo kwa ajili ya mazishi.
Kamanda Nyombi aliwataka madereva kuwa makini wawapo safarini ili kuepusha ajali zisizo za lazima ambazo zimekuwa zikichangia vifo vya watu wengi na wengine kupata ulemavu wa kudumu.
0 Comments