Rais Jakaya Kikwete, mawaziri na viongozi wa wafanyakazi wakiimba wimbo wa Solidarity Forever wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani katika Uwanja wa michezo wa Jamhuri mjini Morogoro. (Picha na Freddy Maro).
RAIS Jakaya Kikwete amewahakikishia wafanyakazi kote nchini kwamba Serikali yake itaendelea kuboresha maslahi yao kila mara uwezo unaporuhusu.
Aidha, ameagiza wizara husika kuhakikisha kazi zinazostahili kushikwa na wazawa, zinabaki mikononi mwao badala ya kufanywa na wageni.
Mbali na hayo, amesema Serikali itaanza kufikiria mambo mbalimbali yatakayowanufaisha wafanyakazi na kuinua hali zao za maisha ikiwemo kuangalia uwezekano wa wafanyakazi kupata mikopo ya gharama nafuu watakayoitumia kununua au kujenga nyumba , vyombo vya usafiri na vya nyumbani.
Rais Kikwete aliyasema hayo wakati akihutubia maelfu ya wafanyakazi na Watanzania kwa ujumla katika sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani kitaifa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
“Haijapata kutokea,” ilikuwa ni kauli yake ya mwanzo alipoanza hotuba yake na kueleza kuwa mchakato unaendelea katika maandalizi ya Bajeti ijayo ya Serikali kuangalia namna ya kupandisha kima cha chini cha mshahara na nafuu nyinginezo.
Mbali na kuweka wazi juu ya azma hiyo, alisema uwezo wa kimapato wa Serikali ndiyo kikwazo kinachopunguza kasi ya kuboresha mishahara ya watumishi wa umma.
Alisema Serikali imekuwa ikichukua hatua za makusudi za kuboresha mishahara ya watumishi wa umma na wale wa sekta binafsi.
Alisisitiza kuwa kilio cha kuboreshewa mishahara na kupunguziwa kiwango cha kodi “tumekipokea kwa uzito unaostahili. Jambo hili mlishalileta siku za nyuma na tumechukua hatua, tunaendelea na tutaendelea kuchukua hatua.”
Rais alitolea mfano wa kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma kimeongezeka kutoka Sh 64,000 kwa mwezi mwaka 2006 hadi kufikia Sh 135,000 kwa mwezi mwaka 2010, ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 107.
Pia aliitaja sekta binafsi kuwa Bodi ya Mishahara ya kisekta zimeundwa na kufanya kazi imeanza kuzaa matunda ambapo kima cha chini kimepanda kutoka Sh 48,000 kwa mwezi hadi Sh 80,000 na mpaka Sh 300,000 kutegemea na shughuli afanyayo mwajiri.
Alisema pamoja na hatua hizo, bado mishahara ya wafanyakazi nchini ni midogo ukilinganisha na gharama za maisha, na Serikali inatambua hoja na haja ya kuendelea kuongeza mishahara mwaka hadi mwaka kufikia pale inapohitajika ya kumudu gharama za maisha.
“Napenda kuwahakikishia kuwa hakuna upungufu wa dhamira wala utashi wa kisiasa wa kufanya hivyo…kwa upande wangu binafsi au wenzangu serikalini, ahadi ninayopenda kurudia leo ni kuwa tutaendeleza kazi tuliyoianza mwaka hadi mwaka,” alisema Rais Kikwete.
“Hata hivi sasa mchakato unaoendelea wa kutayarisha bajeti ya mwaka ujao wa fedha, wahusika wanaangalia namna ya kupandisha kima cha chini cha mshahara na nafuu nyinginezo.”
Alisema changamoto kubwa ni jinsi ya kuongeza zaidi mapato ya Serikali ili kuwa na fedha za kutosha kuwalipa wafanyakazi mishahara inayokidhi gharama za maisha na kubakia fedha nyingine zaidi kwa kuendesha shughuli zake na kuhudumia wananchi.
Alisema katika kipindi hicho, mapato yaliongezeka kutoka wastani wa Sh bilioni 177.1 kwa mwezi mwaka 2005 hadi Sh bilioni 390.7 kwa mwezi mwaka 2010.
Akijibu risala ya wafanyakazi iliyosomwa na Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Nicholas Mgaya, Rais alipongeza mawazo mengi mazuri yaliyokuwemo katika risala hiyo juu ya namna ya kuongeza mapato ya Serikali , kubana matumizi na kuboresha mishahara.
“Mawazo yenu yanashabihiana sana na mawazo yetu na baadhi ya mambo tunayofanya na kufikiria kuyafanya katika kuboresha mapato ya Serikali na maslahi ya watumishi wa umma…tupeni nafasi tufanyie kazi,” alisema Rais Kikwete.
Kuhusu nafuu kwa wafanyakazi, alisema Serikali itaanza kufikiria mambo mbalimbali yatakayowanufaisha wafanyakazi na kuinua hali zao za maisha.
Mambo hayo ni pamoja na uwezekano wa wafanyakazi kupata mikopo ya gharama nafuu watakayoitumia kununua au kujenga nyumba , vyombo vya usafiri na vya nyumbani.
Alisema katika kufikia azma hiyo, kumeanzishwa Mfuko wa Mikopo ya Watumishi wa Umma, sheria iliyopitishwa na Bunge katika mkutano uliopita.
“Vile vile, nimeagiza tutoe kipaumbele kwa ujenzi wa nyumba za kuishi watumishi wa umma hasa wale wa vijijini na vyombo vya ulinzi na usalama ili tuboreshe mazingira yao ya kazi. Ni kazi ambayo tunaifanya hivi sasa ila tunataka tuipe msukumo mkubwa zaidi,” alisema.
Alisema ushirikiano na mshikamano baina ya utatu uliopo yaani wafanyakazi, waajiri na Serikali ni jambo la msingi na hakuna litakaloshindikana na hakuna mfanyakazi wa Tanzania atakayekuwa mtumwa katika nchi yake.
Akizungumzia ajira kwa wazawa, Rais Kikwete alisema, “Katika risala yenu pia, mmelalamikia wageni kupata ajira zinazostahili kuwa za wananchi.
Hayo ni makosa yanayosababishwa na watendaji katika mamlaka za utoaji wa vibali.
“Nakuomba Mheshimiwa Waziri Gaudencia Kabaka na namuomba Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha, Waziri wa Mambo ya Ndani kuhakikisha kuwa maofisa wahusika katika Wizara zenu wanatimiza ipasavyo wajibu wao kuhusu suala hili. Ni dhambi kuacha Watanzania hawana ajira na kuwapendelea wageni pale isipostahili. Nawaomba wafanyakazi msichoke kutoa taarifa ili makosa hayo yarekebishwe.”
Katika hatua nyingine Rais Kikwete amesema hakuna mwananchi atakayezuiwa kutoa maoni yake juu mchakato wa kuandikwa kwa Katiba mpya na kuwaonya watu wanaotaka kuhodhi mjadala huo kwa manufaa yao binafsi.
Alikuwa akijibu hoja ya Tucta kuhusu Katiba ambapo Kaimu Katibu Mkuu wake, Nicholas Mgaya alimpongeza Rais Kikwete kwa kuona mbali na kutoa msimamo wa kuandikwa kwa Katiba mpya.
“Hakuna atakayeachwa katika kushiriki masuala ya kutoa maoni yake juu ya namna ya kuandikwa kwa Katiba mpya…na kila mtu lazima apewe nafasi ya kusikilizwa kutoa maoni yake,” alisema Rais Kikwete.
Aliwataka Watanzania kutotoa nafasi kwa madikteta kuuteka mjadala wa wananchi wanaojitokeza kutoa maoni yao ama kwa kuwazomea au kuanzisha fujo zenye lengo la kutaka kuvuruga mchakato mzima wa ukusanyaji wa maoni ya wananchi.
“Naomba kila Mtanzania ashiriki kujadili Katiba mpya kwa kutoa maoni yake…na msiwape nafasi madikteta kuuteka mjadala huu. Watanzania msikubali kwa kuwa nanyi mna haki zetu,” alieleza.
Hivyo Rais alisema kuwa kwa vile kila mtu anayo haki za kujadili Katiba mpya, Tucta nayo inayo haki ya kuwasilisha maoni ili yaweze kufanyiwa kazi na Kamati ya kuratibu maoni ya mchakato wa kuandikwa kwa Katiba Mpya.
Shirikisho hilo liliipongeza Serikali kwa kukubali maoni ya wananchi kuhusu kurejeshwa tena kwa Muswada wa mabadiliko ya Katiba na tayari Tucta imetoa maoni na mapendekezo kuhusu Katiba mpya.
Rais Kikwete aliwashukuru viongozi wa Tucta kwa mwaliko kwenye sherehe hizo muhimu ambazo alisema zimekuwa ni za kufana kupita kiasi na kuwapongeza Chama cha Walimu Tanzania (CWT) ambao walikuwa ni waratibu wa Mei Mosi mwaka huu.
Awali, TUCTA katika risala iliyosomwa na Mgaya, imeitaka Serikali kuchukua hatua na kushughulikia matatizo na kero za wafanyakazi ikiwemo uboreshaji wa mishahara kwa matumizi ya umeme.
Pia walitaka kuongezwa kwa ajira kwa wazawa badala ya wageni, kuangalia kwa makini ubinafsishaji wa mashirika ya umma, kuboresha pensheni na malipo ya uzeeni na kuongeza ushirikishwaji wa wafanyakazi katika vyombo vya maamuzi.
0 Comments