MAHAKAMA ya Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa, imemtia hatiani na kumhukumu kifungo cha miaka 30 jela na kuchapwa viboko 24, Polikalipo Mwisua (35) kwa kosa la kumnajisi mwanafunzi mwenye umri wa miaka 12.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Rosaria Mugissa alisema
ameridhishwa pasipo shaka ya aina yoyote na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka kuwa mshitakiwa ambaye ni mkazi wa kijiji cha Tamasenga wilayani Sumbawanga, alitenda kosa hilo kinyume cha sheria.
Alisema Mahakama imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela na viboko 24 ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye nia ya kutenda kosa kama hilo.
Awali Mwendesha Mashitaka, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Elija Matiku alidai kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Oktaba 10, mwaka jana saa 2:30 usiku.
Alidai usiku huo wa tukio kijijini Tamasenga, Polikalipo alimshawishi mtoto huyo ambaye ni jirani yake kuingia nyumbani kwake na kumnajisi.
Upande wa Mashitaka uliomba Mahakama kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa kutokana na kuongezeka kwa matukio ya kunajisi kunakofanywa na watu wazima wilayani humo.
Hata hivyo wakati hukumu hiyo ikisomwa, juzi mshitakiwa hakuwepo Mahakamani hapo.
Kutokana na kosa hilo, Hakimu Mgissa alitoa hati ya kukamatwa kwa mshitakiwa huyo ili atumikie adhabu hiyo, kuchapwa viboko 12 siku anaingia gerezani na vingine 12 siku anamaliza kifungo chake.
(Source Habari Leo)
0 Comments