MBUNGE wa Kinondoni, Idd Azzan, amekanusha kuomba radhi kwa uongozi wa CCM Mkoa kutokana na kauli yake aliyowahi kuitoa, kutaka uongozi huo ujivue gamba kwa ajili ya kulinda maslahi ya chama hicho.
Pia amemtaka Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Kilumbe Ng’enda, kuthibitisha kama kweli anauza unga, vinginevyo atampeleka mahakamani kwa madai ya kumchafua yeye, familia yake, pamoja na wapiga kura wake.
Azzan alitoa kauli hiyo jana katika ofisi za CCM tawi la Mchangani kata ya Makumbusho, wakati wa sherehe za kuwapongeza vijana wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) wa wilaya
hiyo, walioibuka na ubingwa katika michezo mbalimbali iliyoandaliwa na umoja huo Mkoa wa Dar es Salaam.
Alisisitiza kuwa viongozi hao wanapaswa wajivue gamba kwa ajili ya kulinda maslahi ya chama hicho.
Katika sherehe hizo zilizohudhuriwa pia na baadhi ya vijana wa CCM kutoka wilaya za Temeke na Ilala, Azzan alisema malengo yake si kuleta mgongano wa maneno ndani ya chama hicho, isipokuwa kuna watu wana chuki binafsi na yeye.
Alisema yeye kama mbunge aliyechaguliwa kwa kishindo na wananchi wa Kinondoni,
anachokiangalia zaidi ni kujenga mshikamano ndani ya chama hicho ili kuendelea kukipa ushindi.
Mbali na kukanusha taarifa hizo, Azzan pia alitangaza kuwania urais mwaka 2025, huku akiwafananisha watu wanaomchafulia katika nafasi yake kuwa ni sawa na ‘fisi anayesubiria mkono wake udondoke’.
“Nitafuata nyayo za Rais Kikwete, yeye alikaa bungeni vipindi vitatu vya kuchaguliwa, na kingine kimoja cha kuteuliwa na baadaye akagombea urais, hiki ni kipindi changu cha pili, itakapofika 2025 nitawania urais kufuata nyayo zake,” alisema Azzan.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Kinondoni, Aron Mwaikambo, aliwataka
wanachama wa chama hicho kudumisha mshikamano kwa lengo la kukijengea heshima ya chama hicho tawala.
0 Comments